SERIKALI kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na
Mafunzo ya Ufundi imewaasa vijana waliomaliza shule kuacha kujibetweka bali
watumie elimu waliyoipata kujitafutia ajira ili kukabiliana na changamoto ya
ukosefu wa ajira nchini.
Kauli hiyo imetolewa jana Jijini Dar es Salaam na Kaimu
Kamishna wa Elimu kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi Teknolojia na Mafunzo ya
Ufundi, Nicholaus Bureta wakati wa ufunguzi wa mkutano wa vijana wa Afrika
unaojadili changamoto zinazowakabili vijana katika nyanja mbalimbali za
maendeleo.
Bureta alisema kuwa Serikali inatoa elimu bora ili
kuhakikisha vijana wanapata uwezo na maarifa yatakayowasaidia kujiajiri hata
wasipopata nafasi za kuajiriwa katika taasisi na ofisi za umma pamoja na
kuitumia elimu hiyo katika kupambana na vitendo vya rushwa.
“Sera ya Elimu na Mafunzo ya
mwaka 2014 inatutaka tuwe na watanzania walioelimika na wenye mtazamo chanya
ambao utahakikisha jamii yetu inabadilika kufikia uchumi wa kati hivyo vijana
msikae kusubiri ajira bali mjifunze jinsi ya kujiajiri kutokana na elimu
mliyoipata mashuleni”, alisema Bureta.
Kwa upande wake Afisa Habari wa Umoja wa Mataifa (UN),
Stellah Vuzo aliwapongeza vijana hao kuamua kukusanyika kuchangia mawazo yao
juu ya matatizo yanayowakabili kwani vijana wana nafasi kubwa ya kuhakikisha
malengo mbalimbali yanatekelezeka.
Aidha, aliongeza kuwa Umoja wa Mataifa umemteua balozi
kijana ambaye anashughulikia ajira za vijana hivyo aliwaomba vijana
walioshiriki katika mkutano huo kuyafikisha mawazo hayo kwa balozi huyo ili
yaweze kupatiwa ufumbuzi.
Naye Mkuu wa Utafiti kutoka Taasisi ya Kupambana na Kuzuia
Rushwa (PCCB), Daniel Pundu alisema kuwa tatizo la rushwa haliwezi kuisha
endapo vijana hawatashirikishwa hivyo amewasisitiza vijana kushirikiana na
Serikali kuchukua hatua za kupambana na rushwa ili kuhakikisha rushwa
inaondoka.
“Tunajua kuwa vijana ndio nguvu
kazi ya Taifa na ndio sababu tunawasisitiza kupambana na rushwa, kwa kulitambua
hilo Serikali imeanzisha vilabu vya wapinga rushwa katika shule za sekondari na
vyuo vikuu vikiwa na lengo la kuhakikisha vijana wanahusika kwenye mapambano
hayo”, alisema Pundu.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni