Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Mhe. George Simbachawene akizungumza na Wakurugenzi wapya mara baada ya kuapishwa mjini Dodoma.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, Mhe.
Angella Kairuki akiongea Wakurugenzi wapya mara baada ya kuapishwa jana mjini
Dodoma. Kushoto ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-Tawala za Mikoa na Serikali za
Mitaa (OR-TAMISEMI), Mhe. George Simbachawene. Kushoto kwa Simbachawene
ni Mkurugenzi mteule wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilimanjaro Bi. Butamo
Nuru Ndalahwa.
Wakurugenzi wapya 13 wa halmashauri wameapa kulinda maadili na kukabidhiwa majukumu ya kufuatilia maagizo ya Rais, Makamu wa Rais na Waziri Mkuu, kwenye maeneo yao na kutoa mrejesho wa hatua za utekelezaji wake.
Kiapo hicho kilihudhuriwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Angela Kairuki aliyewataka kutilia mkazo ufuatiliaji wa maagizo na kupambana na tatizo la watumishi hewa ambao idadi yao imefikia 17,102 waliogundulika katika kipindi cha kuanzia Machi mpaka sasa.
Wakurugenzi hao walioteuliwa hivi karibuni na Rais, John
Magufuli waliapishwa jana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa (Tamisemi), George Simbachawene katika ukumbi wa Tamisemi
mjini Dodoma.
Akizungumza mara baada ya kiapo hicho, waziri Kairuki
aliwataka wakurugenzi hao kutekeleza matamko yote yanayotolewa na viongozi wa
ngazi za juu serikalini, kwa kutoa mrejesho wa utekelezaji wake.
Kairuki aliwataka kufanya kazi kwa bidii ili wawatumikie
wananchi wanaowaongoza.
“Hata kwa wale ambao wanayafuatilia huwa hawatoi mrejesho wa
hatua zilizofikiwa katika kutekeleza matamko hayo, hivyo ninawaomba
mkayatekeleze maagizo na kurudisha mrejesho kwa kiwango kinachotakiwa,” alisema Kairuki.
Pia, aliwataka wakurugenzi hao kwenda kusimamia fedha za
miradi ya maendeleo zinazotolewa na Serikali hadi senti ya mwisho, ili
kuhakikisha inatekelezwa kwa asilimia 100.
Alisema kuna baadhi ya miradi ya maendeleo, inatekelezwa kwa
fedha za Serikali na wakati huo huo inatumia fedha za wafadhili.
Waziri Kairuki aliwataka wakurugenzi walioapishwa kuhakikisha
miradi yote inayotumia fedha za Serikali inasimamiwa ipasavyo.
“Utakuta mradi mmoja unafadhiliwa na pia unatumia fedha za
Serikali, kwa hiyo wafadhili wakija kukagua wanaonyeshwa jengo likiwa
limekamilika na Serikali nayo ikija kukagua inaonyeshwa jengo hilohilo. Nataka
mkasimamie fedha zote za Serikali kwenye mamlaka zenu,” alisema Kairuki.
Alisema kuna baadhi ya maeneo ambako fedha za Tasaf
(mpango wa kunusuru kaya maskini), zimetumika kujengea maabara na kununulia
madawati kinyume na malengo yaliyokusudiwa.
Pia, aliwataka kuhakikisha hatua kali za kinidhamu
zinachukuliwa kwa wakati kwa watumishi waliosimamishwa kazi katika kipindi cha
miezi sita na si zaidi ya hapo.
Alisema mtumishi aliyechukuliwa hatua za kinidhamu ikiwamo
kufukuzwa au kusimamishwa kazi, mchakato wake wote ufanyike ndani ya miezi
sita.
Aliwataka pia wakurugenzi hao kufuata maadili ya viongozi wa
umma, kwani wakikiuka watafikishwa kwenye baraza la maadili ya viongozi wa umma
ambalo kwa sasa limeongezewa meno.
Pia Kairuki aliwataka wakurugenzi hao kusimamia suala la
rasilimali watu, kwani utafiti ulionyesha kuwa asilimia 80 hadi 90 ya watumishi
wa umma ni watoro.
Alisema katika baadhi ya maeneo kuna wakaguzi na waratibu wa
elimu wa kata, lakini hawatembelei shule zao kuona kama walimu wanahudhuria
shuleni au la.
Kadhalika, aliwataka wakurugenzi hao kuachana na tabia ya
kuwatumia viongozi wa Serikali walioko chini yao, kama vile watendaji wa kata,
vijiji na wenyeviti wa vijiji kuwalimia mashamba yao.
Alisema watakaobainika kufanya vitendo hivyo, watachukuliwa
hatua kali za kinidhamu.
kwa upande wake Waziri Simbachawene aliwataka wakurugenzi
hao kwenda kuchapa kazi bila kumwonea yeyote, Aliwaambia kukusanya mapato kiwe ni kipaumbele chao
cha kwanza, kwani kipimo cha mamlaka yoyote kujitegemea ni uwezo wake wa
kukusanya mapato.
Aliwataka wakurugenzi hao kuhakikisha wanawatembelea
watumishi wao wote ili kujua penye upungufu, idadi yao na hata ikiwezekana
kuwajua kwa majina yao.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni