TAARIFA
KWA VYOMBO VYA HABARI
Mkutano
wa 17 wa Dharura wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki
kufanyika Jijini Dar es Salaam
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ambaye pia ni Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ameitisha
Mkutano wa 17 wa Dharura wa Wakuu wa Nchi Wanachama Jumuiya ya Afrika Mashariki
(EAC) utakaofanyika Ikulu, Jijini Dar es Salaam tarehe 09 Septemba, 2016.
Mkutano huo ambao ulitanguliwa na vikao vya maandalizi vya
Makatibu Wakuu na Mawaziri vilivyofanyika Jijini Arusha utajadili agenda kuu
nne ambazo ni:- Mahusiano ya kibiashara na uwekezaji kati ya Jumuiya ya Afrika
Mashariki (EAC) na Umoja wa Ulaya (EU) kupitia Mkataba wa Ushirikiano wa Kibiashara
(EPA).
Agenda zingine ni Kupokea Taarifa ya Mwezeshaji wa
mazungumzo ya Amani nchini Burundi, Mhe. Benjamin William Mkapa, Rais Mstaafu
wa Tanzania; Kupata taarifa ya hatua za kukamilisha uanachama wa Sudan Kusini
kwenye EAC; na Kuapishwa kwa Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki
kutoka Rwanda.
Akizungumzia mkutano huo kwa Waandishi wa Habari, Waziri wa
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga
amesema kuwa mkutano huu umeitishwa kwa dharura ili kuzungumzia agenda hizo
muhimu hususan ile ya nchi wanachama kukubaliana kwa pamoja kusaini au
kutosaini Mkataba wa EPA ifikapo tarehe 1 Oktoba, 2016.
Kuhusu Mkataba wa EPA, Mhe. Waziri Mahiga alisema kuwa
Jumuiya ya Afrika Mashariki ilianza mazungumzo na Jumuiya ya Ulaya ya
kushirikiana kibiashara kupitia EPA miaka 14 iliyopita na kuingia makubaliano
ya awali mwaka 2014.
Alieleza kuwa kwa mujibu wa makubaliano hayo ya awali EU na
EAC zilikubaliana Mkataba huo usainiwe kwa pamoja na nchi zote za Jumuiya mwezi
Julai 2016 kabla ya kuanza utekelezaji wake.
Hata hivyo Tanzania ilitangaza kutosaini makubaliano hayo
kwa sababu mkataba huo unaweza kukwamisha juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano
ya kuifanya Tanzania nchi ya Viwanda na Uchumi wa kati ifikapo 2025.
Aidha, Tanzania inahitaji kujadiliana zaidi na nchi
wanachama ili kujiridhisha kuwa mkataba huo hautoathiri Mkataba ulioanzisha
Jumuiya ya Afrika Mashariki hususan hatua ya mwanzo ya mkataba ambayo ni Umoja
wa Forodha.
Kuhusu nchi nyingine wanachama Mhe. Mahiga alieleza kwamba,
tayari Kenya na Rwanda zimesaini mkataba huo huku Uganda ikisubiri majadiliano
ya nchi wanachama kabla ya kusaini na Burundi ikijitoa kusaini mkataba huo kwa
vile tayari nchi za Ulaya zimeiwekea vikwazo vya kiuchumi.
Imetolewa
na:
Kitengo cha
Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Dar es Salaam, 07
Septemba 2016.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni