Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe
Magufuli leo tarehe 28 Septemba, 2016 amezindua ndege mpya mbili aina ya
Bombardier Dash 8 Q400 zilizonunuliwa na Serikali kwa ajili ya kutumiwa na
Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL).
Uzinduzi wa ndege hizo za kisasa zilizotengenezwa nchini Canada, umefanyika
katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam na
kuhudhuriwa na Viongozi mbalimbali wakiwemo Spika wa Bunge la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mhe. Job Ndugai, Balozi wa Canada hapa nchini Mhe. Ian
Myles, Mawaziri, Wabunge, Viongozi wa Wafanyabiashara, Taasisi mbalimbali na
wadau wa usafiri wa anga.
Kabla ya kuzindua ndege hizo zenye uwezo wa kubeba abiria 76 kila moja, Rais
Magufuli ameshuhudia makabidhiano ya mkataba wa ukodishaji wa ndege hizo kutoka
kwa Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi kwa niaba ya Wakala wa Ndege za
Serikali (TGFA) kwenda kwa Katibu Mkuu Uchukuzi Dkt. Leonard Chamriho kwa niaba
ya Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL).
Taarifa ya ununuzi wa ndege hizo iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi
John Kijazi imeeleza kuwa ndege hizo ni mali ya Serikali na zitakodishwa kwa
Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) kwa lengo kutoa huduma za usafiri wa anga
ndani na nje ya nchi.
Imeongeza kuwa ndege hizo zimenunuliwa kwa kuzingatia kuwa zinafaa kufanya kazi
katika mazingira ya Tanzania ikilinganishwa na ndege nyingine za jamii yake, na
imetaja manufaa hayo kuwa ni pamoja na uwezo wa kuruka na kutua katika viwanja
vya lami na visivyo vya lami, matumizi madogo ya mafuta, kuwa na injini zenye
nguvu zaidi na kubeba mzigo mkubwa.
"Ni dhairi kuwa ndege hizi zitaimarisha mtandao wa huduma za usafiri wa
anga kwa soko la ndani, lakini pia zitaongeza ushindani na kuleta unafuu wa bei
kwa watumiaji wa usafiri wa anga, vilevile zitaimarisha sekta za biashara na
uwekezaji na kuwezesha watalii kutembelea vivutio vya ndani ya nchi"
ameeleza Balozi Kijazi.
Kwa upande wake Rais Magufuli ameelezea kufurahishwa na kutimia kwa ahadi
aliyoitoa ya kununua ndege mpya ili kufufua usafiri wa anga kupitia ATCL na
ameahidi kuwa Serikali imeanza mazungumzo ya kununua ndege nyingine mbili
zitakazofanya safari za ndani na nje ya bara la Afrika ambapo moja itakuwa na
uwezo wa kubeba abiria 160, na nyingine itakuwa na uwezo wa kubeba abiria zaidi
ya 240.
"Kwa sababu fedha za kununulia ndege hizo zote mbili kubwa zipo, tukinunua
ndege ya kubeba watu 240 itakuwa inatoka hapa Dar es Salaam hadi Marekani bila
kutua popote, itaondoka hapa Dar es Salaam mpaka China bila kutua popote ili
watalii wanaotoka China, Marekani, Urusi, Ujerumani na nchi nyingine wasifikie
nchi nyingine, watue hapa moja kwa moja na waangalie maliasili zetu tulizonazo,
utalii wetu upande, na huo ndio mwelekeo wa nchi yetu tunaoutaka" amesema
Rais Magufuli.
Rais Magufuli amewataka Watanzania kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Serikali
katika kuleta mabadiliko yenye manufaa kwa nchi na kuwapuuza watu wanaobeza
juhudi hizo wakiwemo waliobeza ununuzi wa ndege hizo kwa kujenga hoja zisizo za
msingi.
Aidha, Dkt. Magufuli ameitaka Bodi na Menejimenti ya ATCL kufanya kazi kwa
weledi na ufanisi huku akiisisitiza kuondoa kasoro zote zilizosababisha kampuni
hiyo kudorola ikiwemo kuchuja na kuwaondoa wafanyakazi watakaoshindwa kuendana
na mwelekeo unaostahili, wasio waadilifu na waaminifu, wasaliti na wahujumu.
Rais Magufuli pia amewataka Watanzania wote wafanyabiashara, wakulima na
wafanyakazi kusafiri kwa kutumia ndege hizo ili Kampuni ya ATCL ijiimarishe na
iweze kujiendesha badala ya kutegemea ndege za Serikali.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya
Rais, IKULU
Dar es
Salaam
28 Septemba,
2016
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni