Jumapili, 11 Septemba 2016

TETEMEKO LAUWA ZAIDI YA WATU 10 NA KUJERUHI WENGINE 120 KATIKA MIKOA YA KANDA YA ZIWA.


Tetemeko  la ukubwa wa mtikisiko wa kipimo cha Ritcher 5.7 limetokea katika mikoa mitatu nchini na watu zaidi ya 10 wamekufa na wengine 120 wamejeruhiwa huku majengo mengi yakibomoka.

Mikoa iliyoripotiwa kuathiriwa kwa tetemeko hilo ni Kagera, Mwanza na Mara. Pia tetemeko hilo limeukumba mji wa Kampala na Rakai nchini Uganda jana saa 9.27 alasiri.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kagera, Augustine Ollomi alisema tetemeko hilo limetokea saa tisa alasiri na zaidi ya watu 10 wamekufa.

Awali, akizungumza kwa simu kutoka jiijini Dar es Salaam, Kamanda Ollomi alisema watu wanane walikufa na baadaye alisema idadi hiyo iliongezeka na kwamba alipata taarifa kutoka hospitali ya mkoa kuwa wamepokea miili ya watu 10 na wameihifadhi.

Alisema tisa kati ya waliokufa ni wakazi wa Manispaa ya Bukoba na mmoja ni mkazi wa wilayani Karagwe.

Kamanda alisema miongoni mwa majeruhi wamo wanafunzi 15 wa Shule ya Sekondari ya Wavulana Ihungo na wapo katika hospitali ya mkoa wanaendelea kupatiwa huduma. Alisema bado vikosi vya uokoaji likiwemo Jeshi la Polisi na Zimamoto vinaendelea na uokoaji.

Alisema watu waliojeruhiwa na waliokufa wamedondokewa na kuta, vifusi na vyombo vya ndani.

Alisema wengine walikufa kwa mshituko unaosababishwa na shinikizo la damu na nyumba zaidi ya 40 zimeathirika.

“Ni kweli tetemeko la ardhi limetokea na kusababisha uharibifu mkubwa wa mali za watu, vifo pamoja na majeruhi na bado tunaendelea kupokea taarifa zaidi,” alisema Kamanda Ollomi na kuongeza kuwa mpaka jana jioni walikuwa wakiendelea kupokea taarifa kutoka sehemu mbalimbali za mkoa huo kuhusu vifo na majeruhi.

Wakala wa Jiolojia waelezea ukubwa wake
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST), Profesa Abdulkarim Mruma alisema tetemeko hilo ni kubwa kwa nusu ya kipimo cha juu cha Ritcher10 na limezidi kipimo cha chini cha ukubwa wa Ritcher tatu. Alisema limezidi lililotokea Dodoma hivi karibuni.

Profesa Mruma alisema tetemeko hilo limetokea katika mpaka wa Tanzania na Uganda, kilometa 47 kaskazini mwa Bukoba mkoani Kagera na sababu ni mpasuko wa ardhi katika Bonde la Ufa la magharibi karibu kabisa na Ziwa Victoria .

Amewataka wananchi kuchukua tahadhari kwani kwa kawaida linapotokea tetemeko kubwa kama hilo hufuatiwa na matetemeko madogo na ardhi hutulia baada ya siku mbili mpaka tatu. 

“Kwa wakati huu ili kuepuka madhara zaidi, litakapotokea watoke nje ya nyumba na kukaa mbali na miti kwenye uwanja wa wazi na wanaoendesha magari waache mara moja,” alisema Profesa Mruma.

Alisema kwa sasa wataalamu katika kituo chao cha kupimia matetemeko cha Geita wanaendelea kupata takwimu zaidi kutokana na kuwa mpasuko wa tetemeko hilo umekuwa karibu sana na ziwa Victoria na baadaye watatoa taarifa kuhusu tukio hilo kwa undani.



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni