Mbunge wa Jimbo la Pangani Mhe. Jumaa Awesu
akizungumza na wananchi wa Jimbo hilo katika uzinduzi wa Kivuko cha Mv. Tanga
na Gati ya bandari ya Pangani Mkoani Tanga.
Mkuu wa Mkoa wa Tanga Ndg. Martin
Shigella akitoa taarifa ya utekelezaji wa Miradi ya Miundombinu katika Mkoa wa
Tanga kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa katika
uzinduzi wa Kivuko cha Mv. Tanga na Gati Mkoani Tanga.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) Eng.Karim Mattaka akisoma taarifa ya ujenzi wa Gati ya bandari ya Pangani kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa katika uzinduzi wa Kivuko cha Mv. Tanga na Gati Mkoani Tanga.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akifafanua jambo kwa wananchi wa Pangani
katika uzinduzi wa Kivuko cha Mv. Tanga na Gati Mkoani Tanga.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa pamoja na watendaji wa Serikali na
Wizara wakikata utepe kuashiria uzinduzi rasmi wa Kivuko cha Mv. Tanga kulia ni
Mkuu wa wilaya ya Pamgani Mhe. Zainabu Abdallah Issa.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa pamoja na watendaji wa Serikali na
Wizara wakizindua Gati la Bandari ya Tanga Ukamilifu wa Gati hiyo utasaidia
Meli mbalimbali kuweza kutiananga wilayani Pangani.
Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa wa pili kulia
akisafiri na wakazi katika Kivuko cha Mv.Tanga kutoka Pangani kwenda Bweni mara
baada ya uzinduzi, Wanne kushoto ni Katibu Mkuu wa Wizara ujenzi Eng. Joseph
Nyamhanga.
HABARI
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa amezindua kivuko kipya na cha kisasa cha Mv. Tanga kinachotoa huduma ya usafirishaji kati ya Pangani na Bweni na kuzindua Gati ya Bandari ya Pangani wilayani pangani mkoani Tanga.
Akizungumza katika uzinduzi huo Waziri Mbarawa
amesema ujio wa kivuko hicho utafungua fursa za kibiashara na kuchochea
maendeleo ya kiuchumi wilayani hapo.
“Ujio wa kivuko hiki ni mwanzo wa kufunguka fulsa
mbalimbali za kiuchumi kwenu watu wa pangani ,kivuko kitarahisisha huduma za
kijamii na maendeleo ya kiuchumi wilayani hapa, hivyo naomba mkitunze vizuri
kivuko hiki ili kiweze kudumu kwa muda mrefu”, amesema Prof.Mbarawa.
Ameongeza katika kuhakikisha huduma za kivuko
zinakuwepo muda wote wilayani hapo, Serikali kupitia Wizara ya ujenzi imetenga
fedha kwa ajili ya ujenzi wa boti ambayo itatumika kama mbadala wa usafiri
wakati wa usiku katika maeneo hayo ambapo kivuko cha Mv.Tanga hakifanyi kazi.
Kuhusu ujenzi wa Gati ya bandari ya Pangani Waziri
Mbarawa ameseama ujenzi wa gati hiyo utapelekea Meli kubwa kuweza kutiananga na
kurahisisha usafiri wa moja kwa moja kutoka Pangani kwenda visiwa vya Unguja na
Pemba.
Pia amesema Serikali kwa kushirikiana na wadau
mbalimbali wataanzisha huduma ya boti za haraka kutoka Pangani kwenda Mkokotoni
Zanzibar hivyo kufungua fursa za kibiashara na kitalii baina ya Tanga na
Zanzibar.
Kwa upande wa huduma za mawasiliano ya simu wilayani
hapo, Prof. Mbarawa amesema huduma hiyo itaanza mwezi Desemba mwaka huu kwa
mkandarasi kufika na kuanza ujenzi wa miundombinu ya simu na hivyo kuondoa
tatizo la mawasiliano wilayani Pangani.
Katika hatua nyingine Prof. Mbarawa amehahidi kuanza
ujenzi wa Barabara ya Tanga-Pangani-Saadani hadi Bagamoyo (KM 242) kwa kiwango
cha lami ifikapo 2017.
Amesema ujenzi wa barabara hiyo utakuwa wa awamu ili
kuweza kuharakisha kukamilika kwake ambapo awamu ya kwanza itahusisha kipande
cha barabara ya Tanga- Pangani (KM 50) na kuongeza kuwa ujenzi wa barabara hiyo
utafungua fursa za kiuchumi kati ya Tanga na Pangani.
“Naahidi kujenga barabara hii ambayo ni kiungo kati
ya Tanga na Pangani, naamini ukamilifu wake utalete maendeleo mkoani hapa”.
Amesisitiza Prof Mbarawa.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya ujenzi
Eng.Joseph Nyamhanga amezipongeza kampuni za Songoro Marine na Alpha Logistic
kwa kumaliza kwa wakati ujenzi wa kivuko na Gati ya bandari ya Pangani.
Naye Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na
Umeme (TEMESA) Eng. Manase Ole-kujan amesema kivuko cha Mv.Tanga kimejengwa kwa
sh. bilioni nne ambapo kina uwezo wa kubeba tani 50 abiria 100 na magari madogo
6 kwa wakati mmoja.
Ujenzi wa Kivuko cha Mv. Tanga ni moja ya
utekelezaji wa ahadi ya Mhe.Rais Dkt. John Pombe Magufuli aliyoitoa wakati wa
kampeni ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 wilayani Pangani Mkoani Tanga.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni