MKUU wa Mkoa wa
Arusha, Mrisho Gambo ameamuru posho walizokuwa wakilipwa madiwani wa Jiji la
Arusha, zinazofikia zaidi ya mamilioni ya fedha kwa ajili ya vikao, nauli,
mafuta na vocha za simu, kubadilishwa matumizi na kulipa madeni ya walimu
wanaodai zaidi ya Sh milioni 154.
Amesema kila mwalimu
anastahili kusimamia mitihani na kupata posho na si baadhi ya walimu kusimamia
mitihani hiyo mara kwa mara kama vile hakuna wengine.
Uamuzi huo wa Gambo
ameutoa jana wakati alipozungumza na walimu wa shule za msingi na sekondari,
walimu wakuu, waratibu wa elimu kata pamoja na wakuu wa vitengo mbalimbali za
utumishi wa umma akiwemo Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Gabriel Daqqaro na
Mkurugenzi Mtendaji wa Jiji la Arusha, Athumani Kihamia.
Gambo amesema fedha
hizo zilizobadilishwa matumizi yake, zinatoka kwenye posho walizokuwa
wakilipana madiwani hao kwenye sikukuu, ambazo Mkurugenzi wa Jiji aliyekuwepo
kabla ya wa sasa na Meya walikuwa wakilipana Sh milioni moja kila sikukuu, Sh
milioni 61.2 za simu, nauli Sh milioni 28 na gharama za mafuta ambazo wamekuwa
walipwa madiwani hao kulingana na umbali, ikiwemo posho ya dereva anayetoka nje
ya mkoa Sh 100,000 kwa siku na kulipwa kadri ya siku atakazokaa.
Amesema fedha hizo
ni nyingi na hivi sasa zimesitishwa matumizi yake, badala yake madiwani hao
watalipwa Sh 10,000 kama nauli kwa ajili ya kuja kwenye vikao vya Baraza la
Madiwani na posho zao za vikao, ambazo pia zimepunguzwa.
Amesema haiwezekani
walimu wadai zaidi ya Sh milioni 154 ambazo jiji linaweza kuwalipa kulingana na
vyanzo vya mapato vya ndani, badala yake madiwani ndio wanufaike na fedha hizo
huku kila sikukuu wakijilipa posho kubwa na watumishi wengine wakishindwa
kutatuliwa kero zao na kuzungushwa tu.
“Haiwezekani walimu
wawe wanaidai serikali zaidi ya shilingi milioni 154 wakashindwa kulipwa huku
wakifanya kazi kwenye mazingira magumu halafu wengine wanakula raha…sasa nasema
walimu walipwe fedha hizi ndani ya wiki mbili na fedha hizi walikuwa wakilipwa
madiwani sasa nasema walimu walipwe madeni yao ikiwemo malimbikizo ya nauli na
fedha za kupandishwa madaraja,” amesema Gambo.
Amewaagiza mkuu wa
wilaya na mkurugenzi wa jiji kuhakikisha wanakwenda kuangalia shule za
sekondari na msingi na kuzikagua ili kujionea hali halisi sambamba na kuwaagiza
wakuu wa shule mbalimbali za msingi na sekondari kuanisha ni nyumba ngapi
zinahitajika kwaajili ya ujenzi wa nyumba za walimu.
Amewataka wakuu wa
shule za sekondari na msingi kutoa nafasi kwa walimu wengine kusimamia mitihani
na fursa nyingine zinazojitokeza badala ya kufanya upendeleo kwa baadhi ya
walimu ikiwemo kupandishwa madaraja walimu wasiostahili kunakotokana na
kujipendekeza kwa wakuu wa shule au kutoa rushwa ya ngono kupata fursa hizo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni