Waziri wa
Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu ameliagiza
Baraza la Famasia nchini kuanza kazi ya uhakiki wa vyeti vya wauza dawa katika
maeneo mbalimbali nchini kwa lengo la kudhibiti na kuwaondoa wauza Dawa wote
wasio na sifa ya kufanya kazi hiyo.
Pia
ameligiza Baraza hilo kuwachukulia hatua kali za kinidhamu na kisheria ikiwemo
kuwafutia usajili wafamasia wanaokiuka kanuni na taratibu za Baraza hilo ambao
wamekuwa wakijihusisha na vitendo vya upotevu wa dawa, vifaa na Vifaa Tiba vya
Serikali.
Mhe.Ummy
aliyasema hayo jana mjini Dodoma katika Kikao Chake cha kwanza na Bodi ya
Baraza la Wafamasia nchini ambapo pamoja na mambo mengine alikemea utaratibu
ulojitokeza hivi karibuni wa kutaka kuifanya biashara ya dawa kuwa sawa
na biashara nyingine za kawaida za maduka ya kuuza nguo jambo ambalo
halikubaliki.
“Biashara
ya maduka ya dawa lazima iheshimiwe, lazima ianzishwe kwa kufuata taratibu
zinazotakiwa ikiwa ni pamoja na watu wanaoajiliwa kuhudumia maduka ya dawa kuwa
na sifa zinazotakiwa, kazi ya kuuza dawa za binadamu sio sawa na biashara ya
kuuza nguo au viatu”, alisema Mhe Ummy.
Ameliagiza
Baraza hilo kufanya operesheni nchi nzima kukagua maduka yote ya dawa
kubaini mapungufu yaliyopo kisha kuchukua hatua kali dhidi ya wale
wataogundulika kufanya biashara hiyo bila kufuata taratibu na kuongeza kuwa
baraza hilo ni lazima liendelee kupambana na watoa dawa wasio na sifa na
wale wasio waaminifu wanaotengeneza vyeti bandia vya Wataalam wa Famasi.
Pia
ametoa maelekezo kwa baraza hilo kuangalia suala la mgongano wa maslahi
hasa pale ambapo Mfamasia wa Wilaya anatuhumiwa kumiliki maduka ya Dawa mawili
hadi matatu ndani ya Halmashauri anayofanyia kazi.
“Ni
lazima suala hili tulitafutue suluhish nimefanya ziara mikoani jambo hili
nimelikuta, mimi sielewi na Wananchi wengi hawaelewi pale Mfamasia wa Wilaya
anapokua na maduka ya dawa hadi matatu na muda wote yana dawa wakati dawa
hizo hizo hazipatikani katika vituo na Hospitali za Serikal, Kwa nini wananchi
wasiwe na hisia kuwa dawa zile ni za Serikali? Baraza nileteeni mapendekezo ya
kutatua hili. Alisema Ummy.
Aidha,
ameliagiza Baraza hilo kuweka msukumo wa pekee kwenye masuala ya
kuboresha mafunzo na elimu ili nchi iwe na wanataaluma wenye uwezo wa utendaji
wa kiwango cha hali ya juu katika nchi yetu.
Akitoa
Taarifa ya Utendaji Msajili wa Baraza la Famasia Bi.Elizabeth Shekalaghe alieleza
kuwa zipo changamoto wanazokumbana nazo katika kutekeleza majukumu yao ikiwemo
maduka mengi ya kuuza dawa kuendesha biashara hiyo bila ya kuwa na vibali vya
biashaa pia kuwepo kwa wauza dawa wasio na sifa ya kufanya shuguli hiyo.
Pia
alieleza mikakati iliyowekwa na baraza ili kuhakisha changamoto zilizopo
zinapatiwa ufumbuzi ili kuhakikisha huduma za uuzaji dawa zinafanyika kwa
kuzingatia sheria na taratibu ili kuhakikisha ubora wa huduma.
Kwa upande
wake Mwenyekiti wa Bodi ya Baraza la Famasia, Legu Ramadhani Mhangwa, amesema
Baraza limekuwa likifanya kazi zake kwa kuzingatia sheria ili kufikia
malengo iliyojiwekea na kuahidi kuyafanyia kazi maelekezo waliyopewa na Mhe
Waziri pia kutatua changamoto ya uwepo wa vyuo binafsi vinavyofundisha
taaluma ya famasia kutokidhi viwango pamoja na nia ya serikali ya kuongeza
idadi ya wataalamu wa kada za dawa nchini.
Pia
Baraza limeahidi kushughulikia uhaba wa wakufunzi mahususi katika vyuo
vinavyofundisha kada za famasi katika ngazi ya cheti na diploma.
Mwenyekiti
Baraza ameahidi kuhakikisha wanasimamia kikamilifu Kanuni za Maadili na Miiko
ya Kitaalamu za 2015 ili kutatua changamoto zilizojitokeza za upotevu wa madawa
za Serikali.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni