Baadhi
ya waumini wa Roman Katoliki wakifurahi na kuserebuka wakati wa sherehe za maadhimisho ya
miaka 20 ya Redio Maria Tanzania (RMTZ).
Spika Mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Anne Makinda akikata keki wakati wa sherehe za kilele cha maadhimisho ya miaka 20 ya Redio Maria Tanzania leo Jijini Dar es Salaam yaliyoanza rasmi tangu April 26 mwaka huu. Katikati ni Mwashamu Baba Askofu wa Jimbo Katoliki la Mtwara Titus Mdoe,kutoka kulia ni Mhamasishaji Mkuu wa Redio Maria Tanzania Bi. Veronica Mwita na wapili kushoto ni Mkurugenzi wa Redio Maria Tanzania (RMTZ) Padre John Maendeleo
Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu wa
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Benjamin William Mkapa
akisalimiana na Baba Askofu wa Jimbo Katoliki la Mtwara Mwashamu Askofu Titus
Mdoe wakati wa sherehe za maadhimisho ya miaka 20 ya Redio Maria Tanzania leo
Jijini Dar es Salaam.Katikati ni Mkurugenzi wa Redio Maria Tanzania Padre. John
Maendeleo.
Rais wa Redio Maria Tanzania, Humphrey Kira ameiomba
Serikali kurekebisha Sheria ya leseni ya redio za jamii ili ziweze kuwa na
vituo vingi vya kurushia matangazo yake.
Hayo yamesemwa leo na Rais huyo wakati alipokuwa
akisoma risala kwenye sherehe za kilele cha maadhimisho ya miaka 20 ya redio
hiyo yaliyofanyika kwenye viwanja vya Msimbazi Centre, Jijini Dar es Salaam.
Kira amefafanua kuwa redio za kijamii hasa
zilizojikita katika nyanja za kiimani zinasaidia kufundisha maadili na kufanya
wananchi wakomae kiimani, hivyo angefurahi sana kuona redio za aina hiyo
zinapewa leseni za kurusha matangazo yake nchi nzima.
“Ndugu mgeni rasmi, redio yetu inakabiliwa na
changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na ufinyu wa sehemu za usikivu (coverage
areas) ambapo tatizo hili linatokana na sheria ya leseni za redio ambayo
hairuhusu redio za aina hiyo kuwa na vituo zaidi ya kumi nchini nzima, tunaomba
serikali itusaidie kuiboresha sheria hii ili tuongeze vituo vya matangazo ya dini”,
alisema Kira.
Rais huyo ameongeza kuwa majimbo yote yanahitaji
kufikiwa na huduma za maombi, hivyo anawashauri wasikilizaji wote kuendelea
kuisikiliza redio hiyo kwa njia ya mitandao ikiwemo simu za mkononi kwani hivi
sasa huduma hiyo inapatika nchi nzima.
Kwa upande wake Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la
Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo ametoa rai kwa uongozi wa
redio hiyo kutobadilisha maudhui wala kuweka vipindi visivyokuwa vya dini ili
iendelee kuunganisha familia na sio kuzigawa familia.
“Tunasema kuwa redio Maria ni sauti ya kikristu
nyumbani mwako lakini mimi nasema ni sauti ya Mungu ndani ya familia kwa kuwa
inafanya kazi ya kuunganisha familia, vyombo vingine vya habari vinafanya kazi
kubwa ya kuigawa familia lakini Redio Maria ni tofauti”, alisema Pengo.
Askofu Pengo amewashukuru wananchi wote
waliohudhuria kwenye maadhimisho hayo kwa kuwa kufanya hivyo ni njia moja wapo
ya kumuenzi na kumpa heshima Mama Bikira Maria.
Nchini Tanzania, Redio Maria ilianzishwa Aprili 26
mwaka 1996 katika Jimbo Kuu Katoliki la Songea ikiwa na lengo la kumsaidia Mama
Bikira Maria katika kazi yake ya kumtangaza Yesu Kristo kwa watu wote. Mpaka
sasa ina vituo 10 Tanzania Bara na viwili Zanzibar.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni