Bw. Javiero Rielo amesema hayo jana tarehe 24 Agosti, 2016
Ikulu Jijini Dar es Salaam alipokutana na Rais Magufuli kwa lengo la kumpa
taarifa juu ya maendeleo ya maandalizi ya kuanza kwa ujenzi wa bomba la mafuta.
Mradi huo utahusisha ujenzi wa bomba lenye urefu wa kilometa
1,410 ambalo litasafirisha mafuta ghafi kutoka ziwa Albert nchini Uganda hadi
Bandari ya Tanga nchini Tanzania na unatarajiwa kuzalisha ajira za moja kwa
moja 1,500 na ajira zisizo za moja kwa moja 20,000.
Gharama za mradi wa ujenzi wa bomba hilo zinatarajiwa kuwa
takribani Dola za Kimarekani Bilioni 4 na Kampuni ya Total inasema fedha hizo
zipo tayari.
Akizungumza baada ya kupokea taarifa hiyo, Rais Magufuli
amesema anaamini kuwa mradi huo utakuwa na manufaa makubwa kwa Tanzania,
Uganda, Kampuni ya Total na nchi jirani.
Amebainisha kuwa pamoja na kwamba Tanzania ipo katika
mazingira mazuri ya kutekeleza mradi huo, Serikali yake itatoa ushirikiano
mkubwa ili kufanikisha mradi huo.
Katika hatua nyingine, Rais Magufuli amepokea hati za
utambulisho kutoka kwa mabalozi watatu wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini.
Mabalozi waliowasilisha hati zao ni Mhe. Ian Myles – Balozi
wa Canada hapa nchini, Mhe. Prasittiporn Wetprasit – Balozi wa Thailand hapa
nchini mwenye makazi yake Mjini Nairobi nchini Kenya na Mhe. Harald Gunther –
Balozi wa Austria hapa nchini mwenye makazi yake Mjini Nairobi nchini Kenya.
Pamoja na kuwasilisha hati zao za utambulisho Mabalozi hao
wameelezea kufurahishwa na mahusiano na ushirikiano mzuri uliopo kati ya nchi
zao na Tanzania na wameahidi kufanya kazi bega kwa bega na Serikali ya Tanzania
ili wananchi wa pande zote wanufaike na matokeo ya ushirikiano huo hususani
katika uwekezaji na biashara.
Kwa upande wake Rais Magufuli amewahakikishia Mabalozi hao
kuwa Serikali yake itaendeleza na kukuza zaidi ushirikiano kati ya Tanzania na
nchi hizo na ametoa wito kwa Mabalozi hao kuzishawishi zaidi nchi zao na
wawekezaji katika nchi hizo kushirikiana na Tanzania katika ujenzi wa viwanda,
uongezaji thamani ya madini, kuendeleza kilimo hususani kilimo cha umwagiliaji,
uzalishaji wa nishati na biashara mbalimbali.
Pia Rais Magufuli ametoa wito kwa Mabalozi wa Thailand na
Austria kuanzisha ofisi za Ubalozi hapa nchini ili kurahisisha na kuharakisha
shughuli za kibalozi.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es Salaam
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni