Vyeti bandia vya taaluma mbalimbali vilivyo kamatwa
Mihuri iliyokamatwa katika tukio hilo.
Jeshi la polisi mkoani Kigoma limewatia mbaroni watu watano
akiwemo askari mmoja wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kwa
tuhuma za kutengeneza vyeti bandia vya kitaaluma, miongoni mwake vikiwemo 90
vya uuguzi, ambavyo vilikutwa vikisubiri kugawiwa kwa wahusika.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma, Ferdinand Mtui alisema kuwa pamoja na vyeti hivyo vya uuguzi vilivyokamatwa, pia katika operesheni hiyo walikamata vyeti 37 vya wataalamu wa maabara na vyeti tisa vya ufamasia.
Alisema kuwa katika operesheni hiyo iliyofanywa kwa pamoja na
maofisa kutoka Baraza la Wafamasia nchini, walikamata jumla ya vyeti 936 vikiwa
kwenye hatua ya ukamilishaji vikiwa bado havijaandikwa majina, miongoni mwake
vikiwemo vyeti 667 vya wauguzi wasaidizi, vyeti 126 vya wataalam wa maabara,
cheti kimoja cha mafunzo ya afya ya jamii na vyeti viwili vya utoaji huduma ya
kwanza.
Katika kuhakikisha wanakuwa na uthibitisho wa tuhuma hizo,
Kamanda Mtui alisema kuwa pia wamekamata mihuri 25 ya taasisi mbalimbali
ikiwemo nyundo mbili, ambazo hutumika kutengenezea mihuri mbalimbali ya moto.
Aliwataja watu waliokamatwa katika operesheni hiyo ambayo
inahusisha mtandao wa watu mbalimbali kuwa ni askari wa JWTZ, Mgeni Nyamubozi
ambaye ni mume wa mmiliki wa Duka la Vifaa vya Ofisi la Upendo, lililopo Mwanga
mjini Kigoma, ambalo linatuhumiwa kuhusika na utengenezaji wa vyeti hivyo.
Katika duka hilo, Kamanda huyo wa polisi alisema polisi
walikamata kompyuta mpakato moja, ikiwa na nakala za vyeti mbalimbali za vyuo
na idara za serikali.
Mwingine aliyekamatwa ni Dickson Mshahili, muuguzi katika
Hospitali ya Mkoa Kigoma ambaye katika upekuzi nyumbani kwake, alikutwa na
nyaraka mbalimbali ikiwemo madaftari 12 yakiwa na kumbukumbu za vyeti
anavyotengeneza na mihuri ya waganga wakuu wa mikoa ya Kigoma, Kagera, Mwanza,
Singida na Tabora.
Sambamba nao alikamatwa Zawadi James, muuguzi wa Kituo cha
Afya Ujiji ambaye baada ya kupekuliwa nyumbani kwake, alikutwa na vyeti vitatu
na kabuleta ya pikipiki ambayo hutumika kutengeneza mihuri ya moto.
Wengine waliokamatwa ni Johnson Nyabuzoka, mwanafunzi wa
Shule ya Sekondari Mlole ya mjini Kigoma, ambaye ni mtaalam wa kompyuta
aliyekuwa akitumika kufanya kazi hiyo; na Stephano Erasto ambaye alikamatwa
katika siku yake ya kwanza tangu ajiunge na duka hilo kwa ajili ya kusaidia
kazi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni