MATABIBU wanne wa Tiba Asilia na Mbadala akiwemo mmiliki wa
Kliniki ya Sure Herbal, Simon Rusigwa wamewasilisha maombi ya kuomba ruhusa ya
kufungua kesi ya kupinga uamuzi wa kufutiwa leseni za kutoa huduma za kitabibu.
Wamewasilisha maombi hayo katika Mahakama Kuu ya Tanzania
Kanda ya Dar es Salaam, dhidi ya Baraza la Tiba Asilia na Mbadala, Katibu Mkuu
wa Wizara ya Afya na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).
Mbali na Rusigwa, matabibu wengine waliowasilisha maombi
hayo kupitia kwa Wakili Dk Lucas Kamanija, ni Abdallah Mandai wa kliniki ya
Mandai Herbalist, Fadhili Kabujanja wa Fadhaget Sanitarium na John Lupimo wa
Lupimo Sanitarium.
Maombi hayo yalitakiwa kusikilizwa jana mbele ya Jaji
Ama–Isario Munisi wa mahakama hiyo, hata hivyo kabla ya kuanza kusikilizwa,
Serikali iliwasilisha pingamizi la awali ikidai kuwa maombi hayo hayakufuata
misingi ya kisheria.
Katika pingamizi hilo serikali inadai kuwa maombi hayo yana
kasoro kwa kuwa waombaji hawajapita njia zote zinazotakiwa wazifuate ndipo
waende mahakamani pia wanadai maombi hayana miguu ya kusimamia kwa kuwa hati ya
viapo vya walalamikaji vina upungufu ya kisheria.
Baada ya kuwasilishwa kwa pingamizi, Jaji Munisi aliahirisha
shauri hilo hadi kesho saa 8 mchana, ambapo alizitaka pande zote zinazohusika
ziwepo ili kusikiliza pingamizi hilo.
Katika maombi yao, matatibu hao wanadai, wameamua kupeleka
maombi hayo mahakamani, kwa kuwa wanaamini walifutiwa leseni bila kufuata
taratibu za kisheria.
Wamedai wanaamini uamuzi uliochukuliwa umetolewa bila
kupitia Kamati ya Maadili ya Baraza la Tiba Asilia na Mbadala, huku wakidai
kuwa huo si uamuzi bali zilikuwa tuhuma mpya, lakini hawakupewa nafasi ya
kusikilizwa.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni