Jumanne, 16 Agosti 2016

SERIKALI IMEAGIZA HOSPITALI ZOTE NCHINI KUTOA MATIBABU YA UGONJWA WA FISTULA BURE KWA WAKINA MAMA.



SERIKALI imeziagiza hospitali zote za kanda ,rufaa na mikoa kuanza kutoa matibabu bure kwa wakimama ambao ni waathirika wa ugonjwa wa fistula hapa nchi.

Agizo hilo limekuja wakati ambapo tafiti  za kiafya zinaonyesha kuwa gharama kubwa pamoja na uchache wa huduma bora za matibabu ya ugonjwa wa fistula ni kikwazo kikubwa kwa kinamama waathirika wa tatizo hilo.

Hayo yamebainishwa na Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia na Watoto Ummy Mwalimu hapo jana wakati wa uzinduzi wa kambi ya matibabu ya fistula katika hospitali ya bombo yanayoratibiwa na taasisi ya kiislamu ya SMV(sunshine Muslim Volunteers).

Alisema kuwa kutoka na tafiti hizo serikali imejipanga katika kuhakikisha huduma bora za matibabu zinapatikana kwa urahisi kwa waathirika wote kwa gharama nafuu.

“Serikali imeshayaona hayo na hatua zimeshaanza kuchukuliwa kwa kuhakikisha  waathirika wote wanatambuliwa na ikiwemo kupatiwa matibabu haraka kupitia katika maeneo yao waliko”alisema Waziri huyo.

 Aliongeza kuwa serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali inaendelea kuhakikisha kinamama wote waathirika wa tatizo hilo wanapatiwa huduma stahiki bila ya malipo.

 Waziri Mwalimu alisema kuwa kambi hiyo ambayo inajumuisha madaktari bingwa wa kinamama kutoka nchi mbalimbali za ulaya itasaidia kuwajengea uwezo madakrati wa hapa nchi ili waweze kuendeleza juhudi hizo za matibabu.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa taasisi ya SMV Juma Mwimbe alisema kuwa kambi hiyo ina jumla ya madaktari 9 waliobobea katika upasuaji wa fistula kutoka katika nchi za  nchi za Afrika ya Kusini,Canada,Marekani ,Pakistani,pamoja na Uingereza.

Alisema kuwa anaamini kambi hiyo itaweza kutoa huduma bora kwa waathirika wa fistuli walioko katika mkoa huo na mikoa ya jirani kwa ujumla.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni