Madiwani wa Ukawa wa Manispaa ya Kinondoni wamesusa kikao
kilichoitishwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kwa madai
kiongozi huyo hana uhusiano mzuri na viongozi wa upinzani.
Jana, Makonda aliitisha kikao cha wakuu wa wilaya,
wakurugenzi, wakuu wa idara za manispaa za Temeke, Ilala na Kinondoni na
madiwani wote, wakiwamo wabunge wanaounda halmashauri hizo.
Kikao hicho kilichofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa
Arnaoutoglou kililenga kuzungumzia masuala mbalimbali, kama maeneo yaliyovamiwa
na uboreshaji wa elimu mkoani Dar es Salaam.
Akizungumza kwa niaba ya wenzake, meya wa Kinondoni,
Boniface Jacob alisema Makonda amekuwa na tabia ya kudharau na kutoheshimu
viongozi wenzake, hasa wa upinzani akiwaona hawatendi kazi vizuri.
Pia, Jacob alidai kuwa Makonda amekuwa na tabia ya kuingilia
kazi zinazofanywa na viongozi wengine kwa kutumia cheo cha ukuu wa mkoa, jambo
ambalo meya huyo alisema ni kinyume cha sheria.
“Akitaka tumpe ushirikiano, Makonda abadilike la sivyo
mtindo utakuwa huuhuu, mambo yatakuwa hivi. Huu ni mwanzo na ndiyo maana leo
(jana) Ukawa Kinondoni tumekuwa na msimamo mmoja,” alisema Jacob.
Jacob, ambaye pia ni diwani wa Ubungo (Chadema), alisema
hawakuona umuhimu wa kwenda katika kikao hicho kwa sababu kiongozi wa mkutano
huo anawadharau.
Akijibu tuhuma hizo, Makonda alisema madiwani waliohudhuria
kikao hicho maeneo yao yalikuwa na shida na yanahitaji kushughulikiwa, hivyo si
kazi yake kuhesabu watu na kubaini nani hakufika mkutanoni.
Alisema ajenda kuu ya kikao hicho ilikuwa ni kujadiliana
namna bora ya kuvirudisha viwanja vilivyochukuliwa na kuvirejesha kwa matumizi
yaliyokusudiwa.
“Huyo anayelalamika mwambie huo anaoufanya ni utoto akikua
ataacha. Narudia tena siyo kazi yangu kuangalia nani hajaja kwenye kikao,” alisema.
Kwenye kikao hicho, meya wa Ilala (Chadema), Charles Kuyeko
alikuwapo kwenye mkutano huo pamoja na madiwani wenzake, sambamba na wale wa
Temeke.
Makonda si mgeni wa tuhuma .Aliteuliwa kuwa mkuu wa wilaya
ya Kionondoni katika kipindi ambacho alikuwa akituhumiwa kuhusika kwenye sakata
la kupigwa kwa Waziri Mkuu wa zamani, Jaji Joseph Warioba kwenye mdahalo wa
Katiba uliofanyika Hoteli ya Blue Pearl.
Katika kipindi hicho, Makonda pia alikuwa akituhumiwa
kumrushia tuhuma za ufisadi Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa akiahidi kuwa
CCM isingempitisha kugombea urais.
Akitoa majumuhisho ya kikao cha jana kilichoanza saa 2:00
asubuhi hadi saa 5:00 asubuhi, Makonda aliwataka watu waliovamiwa na kujenga
kwenye maeneo yasiyoruhusiwa, kuanza kubomoa majengo yao kabla ya Serikali
kuwafikia.
Kabla ya kutoa majumuisho hayo, Makonda alitoa nafasi kwa
madiwani wa manispaa hizo kueleza kero zinazowakabili, hususan zinazohusu
ardhi.
“Najua mchakato huu utawagusa hadi vigogo, lakini mimi
siogopi vita kwa sababu ndani yangu ninaongozwa na Mungu pekee,” alisema Makonda.
Mbali na hilo, Makonda alisema endapo mtendaji wa ardhi
atayebainika kuhusika katika kuchezea michoro na ramani ili aachie ardhi na
kujipatia fedha, atashughulikiwa kwa mujibu sheria.
Katika hatua nyingine, Makonda amemwagiza kamishna msaidizi
wa ardhi wa Kanda ya Dar es Salaam, Mathew Nhange kumwambia Katibu Mkuu wa
Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi awaondoe maofisa ardhi na
mipango miji wa Kinondoni na Ilala baada ya kushindwa kutoa taarifa za
kuridhisha katika mkutano huo.
Huku akiwataja maofisa hao wanaotoka Kinondoni na Ilala,
Makonda alisema alishakutana na wakuu wa idara kwenye vikao vilivyopita, hivyo
alitegemea kuwa watumishi hao wangetoa taarifa zilizokamilika.
“Kamishna naomba umwambie katibu mkuu mimi siwataki
watumishi hawa katika manispaa hizi. Mwambie awatoe na kuwapangia kazi
nyingine,” alisema Makonda.
Kamishna Nhange alisema agizo hilo analifanyia kazi na kwamba atampa katibu mkuu taarifa za watumishi hao jana
Kamishna Nhange alisema agizo hilo analifanyia kazi na kwamba atampa katibu mkuu taarifa za watumishi hao jana
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni