Siku moja baada ya Rais John Magufuli kuzuia usafirishaji wa
mchanga wa madini kwenda kuuchenjua nje ya nchi akitaka shughuli hizo zifanyike
nchini, imeelezwa kuwa utekelezaji wa dhamira hiyo utachukua muda mrefu
kutokana na mchakato wake.
Rais Magufuli alinukuliwa na vyombo vya habari wilayani
Kahama akisema katika uongozi wake hataki kuona mchanga huo ukisafirishwa hakuna
nchi yoyote yenye madini inayosafirisha
ni Tanzania ndiyo pekee inayosafirisha mchanga kwenda nje hivyo akaagiza
shughuli hiyo ifanyike nchini.
Agizo hilo limekuja wakati utafiti juu ya uwezekano wa
Tanzania kuwekeza katika mtambo wa kuchenjua mchanga wa dhahabu ya uliofanywa
na Wakala wa Ukaguzi Madini Tanzania (TMAA) Februari 2011, ukionyesha kuwa ni
uwekezaji unaohitaji fedha nyingi.
Ripoti hiyo ilisema gharama za usimikaji mtambo kamili wenye
uwezo wa kuchenjua wastani wa tani 150,000 kwa mwaka, ingeweza kufikia Dola za
Marekani 500 milioni hadi Dola 800 milioni (sawa na Sh1.1 trilioni hadi Sh1.74
trilioni za sasa).
Ripoti hiyo ambayo ilikuwa na lengo la kuangalia uwezekano
wa kuchenjua mchanga unaosafirishwa na kampuni ya Acacia inayomiliki migodi ya
dhahabu ya Buzwagi na Bulyanhulu, ilieleza kuwa baadhi ya mataifa
yanayosafirisha mchanga huo kwenda Japani na China ni Chile, Indonesia, Peru,
Marekani, Australia na Canada.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, mgodi wa Barrick (sasa Accacia)
huzalisha na kusafirisha kati ya tani 25,000 na 50,000 za mchanga huo kwa mwaka
ili kuchuja kiwango cha madini yaliyomo.
Akitoa maoni yake binafsi kuhusu agizo hilo, Makamu wa Rais
wa Acacia, Deo Mwanyika alisema msimamo wa Rais Magufuli ni sahihi lakini
utekelezaji wake utahitaji maandalizi kutokana na ukubwa wa gharama za
uwekezaji wa mtambo huo.
Huku akisisitiza kuwa maoni hayo ni yake binafsi, Mwanyika
alisema ipo haja ya Serikali na sekta binafsi kukaa pamoja kwa ajili ya
kujadili shughuli za uwekezaji huo hapa nchini.
“Nimemsikiliza Rais na nimemwelewa dhamira yake lakini
hajamaanisha amezuia rasmi, haiwezekani kuzuia ghafla shughuli hizo. Pia sisi
(wazalishaji) ni tofauti kabisa na sekta hiyo ya uchenjuaji, kwa hiyo itabidi
kujadili nani awekeze, upatikanaji wa mikopo itakuwaje na mambo mengi
yanayohusiana,” alisema.
Serikali iliwahi kulieleza Bunge wakati ikijibu swali la
aliyekuwa Mbunge wa Kahama, James Lembeli, Aprili 2007 kuwa suala hilo ni la
kisera kwa kuwa wawekezaji wameruhusiwa na Serikali ilikwishajitoa kwenye
biashara.
Akijibu swali hilo ambalo Lembeli alitaka kujua kwa nini
mtambo huo usijengwe nchini, aliyekuwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini,
Lawrence Masha alisema hali hiyo imetokana na Serikali kukosa wawekezaji au
wawekezaji kuchelewa kufanya hivyo hapa nchini.
Masha alilishauri Bunge lishirikiane na Serikali kuendelea
kuwakaribisha na kuwashawishi wawekezaji kuja kuwekeza katika mtambo huo wa
kuchenjua mchanga, akibainisha kuwa uwekezaji huo unahitaji mtaji mkubwa.
Miaka kadhaa iliyopita, aliyekuwa Mkurugenzi wa Ukaguzi,
Uzalishaji na Biashara ya Madini wa Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania
(TMAA), Liberatus Chizuzu alikaririwa akisema kuwa gharama za uwekezaji
wa mtambo huo ni kubwa ikilinganishwa na thamani ya mapato yanayopatikana
kupitia uchenjuaji wa madini yaliyopo.
Chizuzu alisema miongoni mwa masharti ya uwekezaji wa mtambo
huo ni upatikanaji wa umeme wa uhakika, jambo ambalo ni changamoto hapa nchini.
Angalizo la Lisu
Juzi, Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu alitoa
angalizo kuhusu hatua hiyo ya Rais akisema Kwa kuzingatia kwamba wawekezaji hao
wanalindwa kisheria na kimkataba.
Mwanasheria huyo mkuu wa Chadema alisema kwa mujibu wa
Sheria ya Madini na Mikataba ya Uendelezaji Madini (MDA), madini yote
yanayochimbwa ni mali ya wawekezaji.
Alisema kwa kuzingatia kwamba wawekezaji hao wanalindwa
kisheria na kimkataba, hatua hiyo inaweza kuwafanya wawekezaji hao kwenda
mahakama za usuluhishi za kimataifa.
Alisema Rais alitakiwa kufanya kama mwenzake, Evo Morales wa
Bolivia ambaye nchi yake ilikuwa na mikataba kama ya Tanzania lakini
alipochaguliwa Desemba, 2006 aliiondoa kwanza kwenye mikataba hiyo iliyokuwa
inailazimisha kuingia kwenye migogoro ya uwezekaji na baada ya hapo ndipo
akabadilisha sheria na mikataba ya uwekezaji iliyoipa Bolivia sehemu kubwa ya
umilikaji wa gesi na mafuta ya nchi yake.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni