Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa
(NIDA) imeeleza kuwa ifikapo Desemba 31 mwaka huu jumla ya watanzania milioni
23 watakuwa na namba za utambulisho wa vitambulisho vya Uraia.
Kaimu Mkuu wa Kitengo cha
Mawasiliano wa Mamlaka hiyo Bi. Rose Mdami amesema kuwa hatua hiyo ni
utekelezaji wa agizo Rais, Dkt. John Pombe Magufuli la kuitaka Mamlaka hiyo
kuweka saini ya mwombaji na mtoaji wa vitambulisho hivyo.
“Tumeanza kutekeleza agizo la Mhe.
Rais tangu mwezi Juni mwaka huu, hii inamaanisha kwamba vitambulisho vyote
tulivyochapisha kuanzia mwezi Juni mpaka leo vina saini ya muombaji, saini ya
mtoaji na tarehe ya kuzaliwa muombaji”
amefafanua Mdami.
Ameeleza kuwa kazi ya ugawaji wa
vitambulisho hivyo inasubiri kuzinduliwa na Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli
atakayekabidhiwa kitambulisho cha uraia namba moja na baadaye
vitambulisho hivyo kugawiwa kwa wananchi wengine.
Mdami amesema ifikapo Desemba 31
mwaka huu NIDA itakuwa imetoa namba za utambulisho wa vitambulisho hivyo
kwa watanzania milioni 23 kwa kutumia taarifa za Tume ya Uchaguzi (NEC) zilizo
katika vitambulisho vya kupigia kura na kuziamishia katika kanzi data ya NIDA.
Amefafanua kuwa ili mwananchi
aweze kupata kitambulisho cha uraia atalazimika kufika katika ofisi za NIDA
akiwa na vielelezo vinavyoonyesha mwaka wake wa kuzaliwa pamoja uthibitisho wa
uraia wake hii ni kutokana na NEC kutokuwa na viambatanisho hivyo.
Amebainisha kuwa mwananchi mwenye
namba ya utambulisho anaweza kupata huduma zote zinazohitaji namba ya
kitambulisho cha Uraia kutokana na namba hiyo kutobadirika na kuendelea
kutumika hata baada ya kitambulisho kuchapishwa.
Amesema mpaka sasa watanzania
milioni 2.7 wamekwisha patiwa vitambulisho hivyo na milioni 6.5
wamesajiriwa kwa ajili ya kupata vitambulisho hivyo.
Aidha, Vitambulisho hivyo vya zamani
vitaendelea kutumika mpaka utakapotangazwa utaratibu wa kuvibadirisha kwa ajili
ya kupata vitambulisho vipya.
Pia ametoa ufafanuzi juu ya
malalamiko ya baadhi ya watu wanaodai kwamba wa kumekuwa na mlolongo mrefu wa
kupata vitambulisho hivyo kwa kueleza kuwa NIDA haina namna ya kufupisha
mlolongo huo kwani kufanya hivyo ni sawa na kuuza uraia wa Tanzania.
Amesisitiza kuwa ni lazima
NIDA ijiridhishe juu ya uhalali na sifa za muombaji ni kuwa ni Mtanzania kwa
kuambatanisha vielelezo vinavyohitajika.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni