Jeshi
la polisi linamshikilia Mwenyekiti wa Mtaa wa Sangabuye, kata ya Igombe wilayani
Ilemela mkoani Mwanza anayejulikana kwa jina la John Mayala kwa kosa la kumtorosha na kumpa ujauzito mwanafunzi.
Mwanafunzi huyo amefahamika kwa jina la Lucy Daudi,
anayesoma kidato cha pili katika Shule ya Sekondari Sangabuye ambaye
anakadiriwa kuwa na umri wa kati ya miaka 14 hadi 17.
Aidha jeshi la polisi pia linamshikilia mama mzazi wa
mwanafunzi huyo aitwaye Agnes Kadilana mwenye umri wa miaka 48 mkulima, mkazi
wa Sangabuye kwa kosa la kushindwa kutoa ushirikiano kwa polisi pindi
alipohojiwa kuhusiana na tukio hilo.
Inadaiwa kuwa mama huyo alishiriki katika kumtorosha binti
yake kwenda kuishi kinyumba na mtuhumiwa baada ya kupewa fedha.
Mama huyo amedai kuwa binti yake aliamua mwenyewe kuacha
shule kwa madai kuwa shule imemshinda. "Yeye mwenyewe alisema hawezi
kusoma, akasema ajifunze cherehani, sasa sijui" Amesema mama huyo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza DCP Ahmed Msangi ametoa
wito kwa wakazi wa mkoa huo hususani wanaume wenye tabia ya kuwa na mahusiano
ya kimapenzi na wanafunzi pamoja na wasichana wenye umri chini ya miaka 18
kuacha mara moja kwani ni kinyume cha sheria bila kujali kama palikuwa na
makubaliano au la.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni