Wakulima wa machungwa Kabuku Wilayani Handeni Tanga
wakiwa katika semina ya kilimo cha machungwa na halizeti wakati wa kujadili
andiko la makabidhiano ya mafanikio wa mradi wa Muunganisho Ujasiriamali
Vijijini (MUVI).
Mkulima wa machungwa Kabuku Handeni Tanga, Rajab Lusewa
akizungumza wakati wa warsha la andiko la makabidhiano ya mafanikio wa mradi wa
Muunganisho Ujasiriamali Vijijini (MUVI).
Mkulima wa machungwa Kabuku Handeni Tanga, Bakari Mgaza,
akizungumza wakati wa warsha la andiko la makabidhiano ya mafanikio wa mradi wa
Muunganisho Ujasiriamali Vijijini (MUVI)
HABARI
MKUU wa Wilaya ya Handeni, Godwin Gondwe, amewataka wakulima wa
machungwa Wilayani humo kutafuta masoko nje likiwamo soko la pamoja la Afrika
Mashariki (EAC) kuepuka kulanguliwa na walanguzi wanaowafuata mashambani.
Akizungumza katika kikao mara baada ya kukabidhiwa mradi wa
Muunganisho wa Ujasiriamali Vijijini (MUVI) kwa halmashauri ya Wilaya hiyo,
Gondwe alisema wakulima wa machungwa wanashindwa kuwa wakulima wa kisasa baada
kushindwa kuthubutu kutafuta masoko nje.
Alisema soko la pamoja na Jumuiya ya Afrika Mashariki lipo
lakini wanashindwa kulitumia badala yake wafanyabiashara kutoka nje wanakuja
mashambani kwao na kununua bidhaa kwa bei ya hasara.
“Kila mtu ndani na nje ya nchi wanajua kuwa Handeni inalima
kilimo cha cha machungwa kwa wingi na wafanyabiashara huja, ila niwaambieni
kuwa munalanguliwa kwa woga wa kwenda kutafuta masoko ” alisema Gondwe na kuongeza
“Soko la pamoja lipo wazi bila vikwazo vyoyote sasa ni kitu
gani kinachotufanya kushindwa kulitumia na kuwaachia wenzetu kuja kwetu na
kutulangua kwa bei ya kutupa hebu jamani tuondoe woga na tuwe tayari” alisema
Pia aliwataka wakulima kuacha woga na badala yake kuwa
tayari kutafuta masoko ndani na nje ya nchi na kuwa wakulima wakubwa na kuacha
kulanguliwa na wafanyabiashara mashambani hii ni fulsa changamkieni.
Akizungumza katika kikao hicho Mwenyekiti wa Wafanyabiasha
wa Machungwa Segera, Hussein Diamballa, aliwataka wafanyabiashara hao kuacha
kuuza machungwa yaliyopepewa na kusema kuwa kufanya hivyo kunaondosha sifa ya
machungwa kituoni hapo.
Alisema kuna wachuuzi ambao wamekuwa wakiuza machungwa
yaliyopepewa na kuchanganya mabovu na hivyo kuwataka kuacha kufanya hivyo kwani
watafanya ukaguzi wa mtu mmoja mmoja.
Alisema umoja huo uko mbioni kusajili wanachama ambao
utakuwa na utaratibu wa kutoa namba na sare hivyo kuwataka kufanya biashara ya
halali na kuacha udanyanyifu.
“Tunataka kuondosha ile dhana ya kituo chetu kuuza machungwa
ya kupepea na kubambika mabovu, hii inatuletea sifa mbaya wakati hapa tunalima
machungwa mazuri yenye maji mengi” alisema Diambala
Aliwataka wafanyabiashara hao kuwafichua wachuuzi wenye
kufanya udanganyifu na kuwaletea sifa mbaya kwa wateja katika kituo cha magari
yaendayo Mikoani kawani wanaweza kuuwa soko ambalo wanaweza kuuza na kupata
mitaji na kuwa wafanyabiashara wakubwa.