Mamlaka ya Udhibiti ya Huduma za Nishati na Maji (EWURA)
imesema ina akiba ya kutosha ya mafuta ya aina mbalimbali yanayoweza kutumika
kati siku 13 hadi 39 nchini.
Mkurugenzi Mkuu wa EWURA, Felix Ngamlagosi, alisema hayo
jijini Dar es Salaam katika mkutano na wadau wa sekta ya mafuta nchini wa
kupokea maoni juu ya mfumo wa uingizaji wa mafuta nchini.
Tamko la EWURA limekuja kukiwa na tatizo la uhaba wa mafuta
ya Petrol, Dizeli na mafuta ya Taa katika baadhi ya mikoa hali iliyosababisha
wananchi wa mikoa iliyokumbwa na tatizo hilo kupata adha.
Ngalamgosi alisema akiba ya mafuta ya ndege iliyopo inatosha
kutumika kwa siku 30 kwa nchini nzima, Petroli ni zaidi ya siku 12, Dizeli ni
zaidi ya siku 15, mafuta ya Taa ni zaidi ya siku 16, mafuta ya Viwandani ni
zaidi ya siku 39 na mafuta ya Migodini zaidi ya siku 13.
Alisema uhaba wa mafuta unaoonekana sasa ulisababishwa na
kuwepo kwa sikukuu zilizofululiza na kusababisha magari ya kubeba mafuta
kushindwa kusafirisha mafuta, na kuyafika kwa wakati katika mikoa hiyo
iliyokubwa na uhaba huo.
Siku ya Jumatano na Alhamisi iliopita palikuwa na siku kuu
za Eid el Fitri.
“Ngalamgosi amewaombe Watanzania wawe na subira kwani
mafuta yapo yakutosha, hivyo nawaomba wasinunue mafuta kwa kupaniki kwani
magari ya kusafirisha mafuta yameanza kusambaza katika mikoa hiyo na hali
itatulia kuanzia sasa,” alisema.
Alisema magari ya mafuta yameshapeleka shehena katika mikoa
ya Mtwara, Ruvuma, Songea na Mbinga ambako hali ya upatikanaji wa mafuta
imeanza kutulia.
Mafuta ya taa
Ngalamgosi alisema uhaba wa mafuta ya Taa ulitokana na meli
iliyokuwa ikishusha mafuta ya Ndege na Petroli kuyachaganya wakati wa
kuyasukuma.
Alisema kuwa kutokana na mchanganyiko huo ni wazi kuwa
mafuta ya Ndege ambayo ndio hutumika kama mafuta ya Taa, hayaweza kutumika kwa
matumizi ya kawaida.
“Mafuta ya Ndege ndio hayo hayo
yanatumika kama mafuta ya Taa hivyo kutokana na kuchanganyika huko ilipaswa
kusafisha matanki yote na mabomba ili kuweka mafuta mapya,” alisema.
Alisema zoezi la kuyasafisha matanki matano lilifanyika kwa
wiki tatu mfululizo na kukamilika Julai 2, kabla ya kuanza kupokea mafuta na
kuyasambaza Julai 3 mwaka huu katika mikoa ambayo kulitokea uhaba.
Kampuni za ndani
Ngalamgosi alisema EWURA imependekeza kubadilishwa kwa mfumo
wa uingizwaji wa mafuta nchini kutoka nchini za nje kwa kuanzishwa mfumo mpya
wa kutoa fursa kwa kampuni za ndani kuingiza mafuta nchini.
Ngalamgosi alisema kuwa amekutana na wadau wa sekta ya
mafuta ili kupokea maoni ni namna gani wanaweza kuboresha ushindani na
wamependekeza kuwa kila meli inayokuja lazima iwe na zabuni yake.
Alisema Tanzania inaingiza meli sita za mafuta kwa mwezi,
hivyo EWURA imeona kuwa inapasa kuwa kila meli ya mafuta inayoingia iwe zabuni
inayojitegemea.
“Kwa kufanya hivyo kutatoa fursa
kwa watanzania kuweza kuingiza mafuta kwa sababu itapunguza gharama na uzuri
utakuwa nchi itanufaika kuwa na watanzania wengi kushiriki katika kuingiza
mafuta,”alisema.
Aliongeza kusema kupita utaratibu mpya wanaamini kuwa Makampuni
ya Tanzania yatapata faida kubwa na TRA kukusanya mapato mengi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni