MCHAKATO wa ujenzi wa mradi mkubwa wa Reli ya Kati nchini kwa kiwango
cha kisasa ‘Standard Gauge’, umeanza rasmi baada ya Serikali ya
Tanzania kusaini mkataba wa ushirikiano (MoU) na Benki ya Exim ya China.
Mkataba huo ulisainiwa katika ofisi za Wizara ya Fedha na
Mipango na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dk Servacius Likwelile na Naibu
Meneja wa Kitengo cha Mikopo Nafuu wa Benki hiyo, Zhu Ying.
Akizungumza baada ya kusaini mkataba huo wa ujenzi wa kilometa 2,190
za reli, Dk Likwelile alisema mkataba huo ni makubaliano ya pamoja ya
matayarisho mbalimbali, ikiwemo kupata sehemu ya fedha za ujenzi huo na
kugawana majukumu ya kila mmoja.
Alisema katika kufikia malengo waliyojiwekea, ikiwemo ya ushirikiano
katika kuleta mapinduzi ya viwanda, kutaundwa kikosi kazi cha pamoja,
kwa ajili ya kushughulikia masuala ya miradi mbalimbali inayofadhiliwa
na benki hiyo.
Miongoni mwa mambo yatakayoshughulikiwa na kikosi kazi hicho, ni kuandaa mradi kwa kuangalia masuala ya kiutawala na
kiufundi na kusimamia kufanyika kwa upembuzi yakinifu na kufungua fursa
mbalimbali.
Dk Likwelile alisema mradi huo mpaka utakapokamilika, unatarajiwa
kugharimu zaidi ya Sh trilioni 16, ambapo reli hiyo ya kiwango cha
kisasa (Standard Gauge), itatoka Dar es Salaam – Tabora –Isaka – Mwanza;
Tabora – Mpanda –Kalemela; Tabora – Uvinza – Kigoma na Isaka – Keza –
Msongati.
Alitaja njia mpya zilizopendekezwa kuwa ni Isaka-Keza –Kigali
(Rwanda) nyingine ni Isaka-Keza-Gitega (Burundi ); Mpanda-Karema, Uvinza
–Musongoti; Mtwara-Songea-Mbambabay mpaka Liganga na Mchuchuma na
Arusha-Musoma.
Awali, Rais wa Benki ya Exim ya China, Liu Liang alipokutana na
kufanya mazungumzo na Rais John Magufuli, alikubali benki hiyo kuchangia
katika ujenzi wa reli iyo ya kisasa ikiwa ni pamoja na kubadilishana
uzoefu na utaalamu katika ujenzi na uendeshaji wa reli.
Katika mazungumzo hayo Rais Magufuli alisema mradi huo utagawanywa
vipande kwa wakandarasi wanne hadi watano, kwa lengo la kuharakisha
ujenzi huo na tayari utaratibu wa kupata wakandarasi hao toka nchini
China umeanza.
Alisema serikali imetenga katika bajeti ya mwaka huu Sh trilioni moja
kwa ajili ya ujenzi wa reli hiyo, ambapo Rais Magufuli alibainisha kuwa
utekelezaji wa mradi huo utasaidia kuinua uchumi wa Tanzania na nchi
jirani zisizopakana na Bahari ya Hindi, ikiwemo Uganda, Rwanda, Burundi
na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni