Jumamosi, 29 Aprili 2017

WAANDISHI WA HABARI MKOA WA TANGA WAFANYA ZIARA KUJIONEA UCHAFUZI WA MAZINGIRA KWENYE VYANZO VYA MAJI.

Waandishi wa habari wa vyombo mbalimbali mkoani Tanga wafanya ziara kutembelea mitambo ya maji ya Tanga Uwasa kuona hali inayosababisha maji kutoka na rangi na kulalamikiwa na wateja wa mamlaka hiyo.
Mratibu  Mazingira wa Mamlaka ya maji na usafi wa mazingira (Tanga Uwasa) Nyambuka Ramadhani akiwaeleza waandishi wa habari jinsi hali ya tope ilivyoingia kwa wingi katika mitambo ya mamlaka hiyo na juhudi za kutibu maji zinazofanywa ili wateja kupata maji safi na salama.
Hili ndiyo bwawa la mabayani linalotengewa na mamlaka ya maji Tanga likiwa limechafuka vibaya kutokana na shughuli za  uchimbaji wa madini unaoendelea katika vyanzo vya maji
Baada ya ziara ya kujionea changamoto zinazoikumba mamlaka ya maji mkoa Tanga  Waandishi wa habari wa vyombo mbalimbali mkoani Tanga kukutana na uongozi  wa Tanga Uwasa kupata majibu ya kile walichojiona katika ziara yao kwenye vyanzo vya maji .
 Afisa wa Uhusiano wa Mamlaka ya maji Tanga(Tanga Uwasa) Dorah Killo akizungumza katika kikao cha viongozi wa Mamlaka hiyo na Waandishi wa Habari wa Tanga baada ya ziara.

Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya maji Tanga ,(Tanga Uwasa) Injinia Joshua Mgeyekwa akizungumza na Waandishi wa habari wa Tanga baada ya ziara yao ya kutembelea vyanzo vya maji na mitambo ya kusafishia maji Jijini Tanga. 
TANGA
MAMLAKA ya Majisafi na Majitaka Jijini Tanga (Tanga-Uwasa), imewahakikishia watumiaji wake wa maji katika Jiji hilo, kwamba pamoja na maji kuja na rangi tofauti kulikosababishwa na tope kuingia kwenye bwawa lililopo Mabayani, bado maji hayo ni safi na salama kwa matumizi ya binadamu.

Akizungumza na Waandishi wa habari mara baada ya kutembelea bwawa hilo pamoja na mto Zigi unaoingiza maji kwenye chanzo chao, Mkurugenzi Mtendaji wa Tanga-Uwasa, Injinia Joshua Mgeyekwa, alikiri kuwa wateja wao wameathirika na uhaba wa maji pamoja na kubadilika rangi kulikosababishwa na tope kuingia kwenye mabomba yao.

“Ni kweli wateja wetu wameathirika na huduma yetu, kutokana na maji yanakuja kidogo na tope…Sababu ya kuwa na tope ni kutokana na maji yanayoingia bwawani kuwa na tope jingi,” alisema Injinia Mgeyekwa.

Alisema kuanzia Machi 28 hadi Aprili 5 mwaka huu, maji yenye tope yaliingia kwa kasi katika bwawa lao la Mabayani na kusababisha pump zinazochanganya  dawa ya kusafisha maji hayo kuzidiwa uwezo na hivyo kiasi cha tope kupenya kwenye mabomba na kuingia kwa watumiaji.

Mgeyekwa alifafanua kwamba kwa kawaida Tanga-Uwasa, inasafisha maji kwa wastani NTU 300 zilizowekwa dawa lakini kutokea mabadiliko ya maji na kusomeka kiwango cha NTU 400 hadi 600 ndiyo aliyosababisha kupitisha tope.

“Uwingi wa tope tunaloweza kulisafisha kwa wastani wa kiasi cha NTU 300 lakini tukakuta imefikia kiasi cha wastani wa NTU 400, 500 hadi 600 kilikuwa kinabadilika wakati umeweka dawa za wastani wa NTU 300 lakini inakuja hadi 600 hii inatokana na mabadiliko ya mara kwa mara,” 

“Ni sahihi wateja wetu walalamike sababu hawajazoea kutumia maji ya aina hiyo, ni sawa walalamike na sisi imetupa changamoto kubwa hasa baada ya kutokea hali hii na utajitahidi kulitatua kadiri tutakavyoweza,” alisema Injini Mgeyekwa.

Hata hivyo, Injinia Mgeyekwa ambaye alikuwa nchini Afrika Kusini kuhudhuria mkutano wa Mamlaka zinazosambaza maji kwa kiwango bora barani Afrika, alisema kuwa tayari wameagiza pump na dawa nyingine kutoka Afrika Kusini ambayo itakuwa na uwezo wa kusukuma tope jingi kwa kiwango kikubwa pamoja na uchanganyaji wa dawa hiyo katika kipindi cha muda mfupi zaidi.

“Tumeanza kutafuta dawa ambazo zitaweza kusafisha maji yenye tope jingi na kwa muda mfupi lakini pia tumeagiza ‘pump’ mpya ya kusukuma tope na kusafisha kwa muda huo mfupi pia tunajua mashine hizi zipo na tutazipata ingawa ni za gharama kubwa lakini tutahakikisha wateja wetu wanapata huduma nzuri,na kwa wakati” alisema Injinia Mgeyekwa.

Akijibu swali kuhusu usalama wa maji yanayosambazwa yakiwa na rangi ya tope, Mkurugenzi huyo alisema kwamba wanajitahidi kwa kiasi kikubwa kuyatibu kuua wadudu ila maji ni salama kwa matuminzi ya binadamu.

“Sisi kuna vitu vitatu huwa tunavitazama ni maji yawe safi, salama kwa matuminzi ya binadamu na tatu ni maji hayo yapaikane ya kutosha kwa wateja wetu,” alisema na kuongeza kwamba hivi sasa wamejaribu kusambaza maji hayo kwa masaa 24 na baadhi ya maeneo ya Jiji la Tanga wanapata maji kwa masaa manane.

Hata hivyo, mkurugenzi huyo alisema kwamba Tanga-Uwasa tangu tatizo hilo lijitokeze wamekuwa wakipata hasara ya karibu shilingi milioni 13 kwa siku kutokana na kushindwa kukusanya malipo ya maji kwa wateja wao baada ya uzalishaji kwa sasa kupungua kutoka lita za ujazo zipatazo 29,500 hadi sasa wanazalisha lita 20,000.

Aidha alisema kwamba kwa upande wa madawa wanayotumia wanapata hasara ya sh. 600,700 kwavile sasa wanatumia shilingi milioni 2.2 badala ya shilingi milioni 1.6.

Akizungumzia picha zinazosambazwa kwenye mitandao kuonesha hali ya maji ya mamlaka hiyo inayosambaza kwa sasa, Mgeyekwa alisema siyo kweli kama ni maji ya mamlaka hiyo bali ni watu wameamua kupotosha wakitumia tatizo hilo lililojitokeza kwa sasa.

Aliwataka wananchi wa Jiji la Tanga kufika katika ofisi ya mamlaka hiyo kuanzia siku ya Jumanne ambapo watafungua dawati la kusikiliza kero zilizosababishwa na tatizo hilo na kuyatolea ufafanuzi lakini pia kujua ili waweze kwenda huko kutatua tatioz hilo.

Maelezo hayo yaliyotolewa na Mkurugenzi huyo yanatokana na ziara ya waandishi wa habari ambao walienda kutazama bwawa la Mabayani ambalo maji yake yamekutwa yakiwa na rangi na kisha baadaye kwenda katika eneo la kijiji cha Kwamtili kilichopo wilayani Mkinga ambako kuna mto Muzi unaoingiza maji kutoka kwenye Mto Zigi.

Katika mto huo waandishi waliwakurupusha baadhi ya wachimbaji wakichimba dhahabu katika mto huo ambao husababisha tope kuingia kwenye mto Zigi ambao hutiriisha maji kwenye bwawa linalotegemewa na Mamlaka hiyo.

Mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira mkoa wa Tanga,(Tanga Uwasa) imetoa onyo kali kwa wanaoharibu vyanzo vya maji kwa kuchimba madini katika mto Muzi na Semdoe kata ya Bosha kijiji cha Kwezitu Wilayani Mkinga.

kwa sasa mamlaka ya maji Tanga imeweka mikakati ya kufufua visima vilivyokuwa vinatumika zamani ili kusaidia upatikanaji wa maji na sasa kisima kimoja kimeshaanza kazi kwa kuhudumia maeneo ya Nguvumali na mengine ya jirani na eneo hilo.

"lengo la mamlaka ni kuondokana na kutegemea bwawa peke yake kwani kwa kipindi hiki tumejifunza mengi hivyo imebidi tuhakikishe mbinu nyingine mbadala zinafanikiwa ili wateja wetu wanaendelea kupata huduma yetu ubora" alisema Injinia Mgeyekwa.

 Mgeyekwa amewaomba radhi wateja wa Tanga Uwasa kwa hali iliyojitokeza ya  ukosekanaji wa maji kwa kipindi cha takribani mwezi mmoja na nusu na maji kutoka yakiwa na rangi.


                                                    

                                 MWISHO







Hakuna maoni:

Chapisha Maoni