Rais wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amepokea kwa
mshtuko na masikitiko makubwa taarifa za vifo vya Askari Polisi 8 waliouawa kwa
kushambuliwa na watu wenye silaha jana jioni katika eneo la Jaribu Mpakani,
Wilaya ya Kibiti Mkoani Pwani.
Askari Polisi hao walikuwa wakitoka kubadilishana doria na
wameshambuliwa kwa kupigwa risasi wakiwa wanasafiri kwa gari katika barabara ya
Dar es Salaam – Lindi.
Mhe. Rais Magufuli amemtumia salamu za rambirambi Mkuu wa
Jeshi la Polisi nchini IGP-Ernest Mangu, familia za askari wote waliouawa,
Askari Polisi wote na Watanzania wote walioguswa na vifo hivyo.
“Nimeshtushwa na nimesikitishwa sana na vifo vya askari wetu
8 ambao wamepoteza maisha wakiwa wanalitumikia Taifa, naungana na familia
za marehemu wote, Jeshi la Polisi na Watanzania wote katika kipindi hiki kigumu
cha huzuni na majonzi ya kuondokewa na vijana wetu shupavu.
“Namuomba Mwenyezi Mungu atupe moyo wa subira, uvumilivu na
ustahimilivu” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Aidha, Mhe. Dkt. Magufuli amelaani tukio hilo na matukio
yote ya kuwashambulia askari polisi ambao wanafanya kazi kubwa na muhimu ya
kulinda raia na mali na ametaka Watanzania wote watoe ushirikiano katika
kukomesha vitendo hivyo.
Mhe. Rais Magufuli amewaombea marehemu wote wapumzishwe
mahali pema peponi, Amina.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni