WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewaomba viongozi wa
dini nchini kutumia nafasi zao kuhimiza wazazi na walezi kuishi maisha yenye
nidhamu, kuthamini kazi yenye kumpendeza Mwenyezi Mungu na kusimamia malezi ya
watoto na kuzingatia maadili ya Taifa kwa ujumla.
“Tabia na mwenendo mzuri ni lazima uanzie katika
ngazi ya familia, mtaani na hatimaye katika jamii. Tukirudia utamaduni wetu wa
zamani wa kusimamia maadili kwa pamoja, jamii yetu itanusurika kwa kiwango
kikubwa,” amesema.
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Jumatatu, Aprili
24,2017) wakati akifungua kongamano kuhusu mmomonyoko wa maadili na athari za
dawa za kulevya lililoandaliwa na Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) kwa
kushirikiana na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya,
lililofanyika mjini Dar es Salaam.
Amesema kila mzazi au mlezi aone aibu, uchungu na
ajutie anapoona mtoto yoyote akienda kinyume na utaratibu wa kawaida wa maisha
na ni vema wakatumia nafasi yao kwa kuwahimiza vijana hao waishi maisha ya
nidhamu na yenye kumpendeza Mwenyezi Mungu.
Waziri Mkuu amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Tano
imedhamiria kujenga jamii yenye kuzingatia maadili nchini na Mheshimiwa
Rais, Dkt. John Magufuli amekuwa akiwasisitizia Watanzania wote kuzingatia
maadili katika jamii kwa kufanya kazi kwa bidii na kujiepusha na vitendo vyote
vya rushwa na ubadhirifu.
Amesema maadili katika Taifa ni moja ya tunu muhimu
kwa kuwa ndicho kichocheo kikubwa cha maendeleo, ujenzi wa umoja, amani,
upendo, uvumilivu na mshikamano kwa jamii.
Amesema maadili ni nyenzo muhimu sana katika ujenzi
wa Taifa na huliepusha kuingia katika mifarakano na migogoro. “Hivyo hatuna
budi nasi kuyalinda maadili hayo kwa uwezo wetu wote, ili tuyarithishe kwa
vizazi vijavyo, kama vile sisi tulivyoyarithi kutoka kwa waasisi wa Taifa letu,”.
“Hata hivyo, ninyi ni mashahidi kuwa katika siku za
hivi karibuni tumeshuhudia vitendo vya mmomonyoko wa maadili na matokeo yake
yanaonekana dhahiri kama kuongezeka kwa vitendo vya rushwa, kuiga tamaduni za
nchi za kigeni ambazo sio njema na hazina tija kwa jamii, na Taifa kwa ujumla”.
“Ni ukweli usiopingika kuwa mmomonyoko wa maadili ni
miongoni mwa vichocheo vinavyopelekea matumizi ya dawa haramu za kulevya. Hivyo
ni matarajio yangu kuwa mtaliangalia kwa kina tatizo la mmomonyoko wa maadili
ambalo kwa kiasi kikubwa linatuathiri kama Taifa katika mipango ya Serikali na
maendeleo ya Taifa letu,” amesema.
Hivyo Waziri Mkuu amewapongeza viongozi wa BAKWATA
kwa kuwa na wazo la kufanya kongamano hilo lenye kulenga kujadili namna ya
kurejesha maadili katika jamii. Tukumbuke kuwa Watanzania tutaendelea kuishi
kwa upendo, amani na utulivu iwapo tutazingatia maadili.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema Serikali
ya Awamu ya Tano ipo mstari wa mbele kuhakikisha kuwa mapambano na vita dhidi
ya dawa za kulevya nchini inafanikiwa. Lengo ni kuhakikisha kuwa waathirika
wote wa matumizi ya dawa hizo wakiwemo vijana, ambao ndio nguvu kazi ya Taifa
wanakombolewa dhidi ya janga hilo.
Amesema Serikali itahakikisha inashughulikia mtandao
wa wafanyabiashara wakubwa wanaojihusisha na dawa za kulevya bila ajizi, ambapo
vyombo vyote vya kisheria vimeelekezwa kushirikiana katika mapambano dhidi ya
matumizi ya dawa ya kulevya kwa kusimamia sheria ipasavyo.
Naye Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na
Kupambana na Dawa za Kulevya nchini, Bw. Rogers Siyanga amewaomba viongozi wa
dini kuiunga mkono mamlaka hiyo kwa sababu inafanya kazi kubwa ambayo inahitaji
msaada wa watu wote.
Kwa upande wake Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania,
Alhaji Abubakary Zuberi amesema viongozi wa dini nchini wana jukumu la kukataza
maovu na kuiamrisha jamii kufanya mambo mema badala ya kuiachia Serikali pekee
kufanya kazi hiyo.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMATATU, APRILI 24, 2017.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni