Serikali imepokea kwa masikitiko taarifa za
kushambuliwa na kujeruhiwa baadhi ya waandishi wa habari katika mvutano
uliotokea juzi jijini Dar es Salaam kati ya wafuasi wa pande mbili
zinazokinzana za Chama cha Wananchi (CUF). Tumechukua muda kidogo kulifuatilia
suala hili na kubaini licha ya baadhi yao kujeruhiwa na kuripoti polisi, wapo
waandishi ambao vifaa vyao vya kazi pia vililengwa katika shambulizi hilo.
Tunachukua fursa hii kulaani kitendo cha kuumizwa
wanahabari tena waliokuwa wamealikwa kuhudhuria mkutano huo. Ifahamike kuwa
uandishi wa habari ni taaluma adhimu na nadhifu inayopaswa kuheshimiwa,
kuenziwa, kulindwa na kutoingizwa katika migogoro ya pande zinazofarakana
katika jamii.
Kifungu cha 7 (1) (a) cha Sheria ya Huduma za Habari
Na. 12 ya mwaka 2016 kinaainisha uhuru wa wanahabari katika kukusanya habari
kwa muktadha wa kuwepo katika maeneo ya matukio kama hakuna sababu nyingine za
kuzuiwa. Misingi ya uhuru huu wa kitaaluma pia imesisitizwa katika Ibara za 18
ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977 na 19 ya Mkataba wa
Kimataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa wa mwaka 1966 ambao nchi yetu
imeuridhia.
Tunawatakia nafuu ya haraka wanahabari waliojeruhiwa
na wenzao wengine waliopatwa na jakamoyo katika tukio hilo. Kwa kuwa suala hili
tayari limeripotiwa polisi, tunawaomba wadau wote wa habari na wanasiasa kwa
sasa kutulia na kuviachia vyombo husika vilifanyiekazi ili hatua stahiki za
kisheria zichukuliwe.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni