WAKATI Rais John Magufuli alitishia kubadili fedha za
Tanzania katika juhudi za kuwadhibiti watu wanaodaiwa kuficha fedha, Waziri
Mkuu wa India, Narendra Modi ametangaza kuziondoa kwenye mzunguko noti za Rupia
500 na 1,000.
Akizungumza katika mkutano wa 14 wa mwaka wa wahandisi
uliofanyika Septemba Mosi katika Ukumbi wa Mlimani City, Rais Magufuli alisema
kwa mamlaka aliyonayo anaweza kuamua kubadili fedha ili zile zinazofichwa, watu
hao wakose mahali pa kuzipeleka.
Alisisitiza kwa kusema kauli hiyo ni mahsusi kwa watu
walioficha fedha katika majumba yao na kuwataka kuacha tabia hiyo mara moja ili
fedha hizo ziingie katika mzunguko.
Rais Magufuli alisema katika utawala wake fedha za bure
hazitakuwapo kwa sababu zilizokuwapo awali zilitokana na fedha za wizi kutoka
serikalini ambazo kwa sasa zimedhibitiwa.
Alisema kwa mwendo anaokwenda nao sasa ni ngumu kwa
mwananchi kupata fedha bila kufanya kazi.
Habari kutoka India zinasema Waziri Mkuu Modi alitangaza
hatua hiyo ya kushangaza kwenye runinga Jumanne usiku kuwa ni mojawapo ya
harakati za kukabiliana na ufisadi na ukopeshaji wa fedha haramu.
Modi alisema noti zote za Rupia 500 na 1,000 “hazitakuwa
fedha halali kuanzia usiku wa manane leo” na kwamba “zitabaki kuwa makaratasi
yasiyo na maana.”
Hata hivyo, alisema noti nyingine za Rupia 100, Rupia 50,
Rupia 20, Rupia 10, Rupia 5, Rupia 2 na sarafu zote zitaendelea kuwa na
thamani.
“Ulanguzi wa fedha na ufisadi ndiyo vikwazo vikuu katika
kukabiliana na umasikini,” alisema Modi na kuongeza: “Watu wataweza kubadilisha
noti zao za zamani na mpya katika benki kuanzia Novemba 10 hadi Desemba 30 na
kwamba fedha hizo hazitatumika tena.”
Benki zilifungwa jana huku huduma za mashine za kutoa pesa
za ATM zikisitishwa. Badala yake noti mpya za Rupia 500 na 2,000 zitawekwa
katika mfumo wa fedha kuchukua nafasi ya zilizoondolewa.
Tangazo hilo lilisababisha mtafaruku kwenye vituo vya mafuta
na maeneo mengine ya biashara kwani wauzaji wa rejareja walikuwa wakikataa
kupokea noti hizo huku mashine za kutolea fedha zikifungwa. Katika viwango vya
ubadilishaji fedha noti ya Rupia 500 ni sawa na Sh16,000 na Rupia 1,000 ni sawa
na Sh32,000.
Wateja watakuwa na uwezo wa kubadili noti hizo ili wapewe
mpya au kuziweka kwenye akaunti, lakini watatakiwa kujieleza mamlaka ya mapato
walivyozipata.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni