Wanafunzi wa kidato cha pili nchini wameanza kufanya
mitihani yao ya upimaji leo katika shule za sekondari 4,669 zilizopo Tanzania
Bara.
Jumla ya wanafunzi 435,221 wamesajiliwa kufanya mitihani
hiyo wakiwamo 67 wasioona na 306 wenye uoni hafifu.
Mbali na mitihani hiyo, Katibu Mtendaji wa Baraza la
Mitihani la Taifa (Necta), Dk Charles Msonde amesema mtihani wa Taifa wa darasa
la nne utafanyika Novemba 23 na 24, mwaka huu.
"Mitihani hii inafanyika katikati ya mafunzo ili
kubaini changamoto zilizopo na kutafuta namna ya kuboresha mafunzo hayo,"
amesema Dk
Msonde.
Wakati huo huo, Dk Msonde amefafanua kuwa mafunzo ya ualimu
wa shule ya msingi ngazi ya stashahada yamefutwa lakini wanafunzi waliopo
vyuoni watamalizia masomo yao kwa muda uliobaki.
Dk Msonde amesema mafunzo hayo ya walimu yataendelea kwa
utaratibu wa zamani ambao ulikuwa ngazi ya cheti.
Amesema usimamizi wa mitihani hiyo itakuwa chini ya Necta
kama ilivyokuwa zamani badala ya Nacte.
"Wanafunzi walio vyuoni wataendelea na mafunzo hayo,
isipokuwa kuanzia mwaka huu hatutadahili kwa ngazi ya diploma, tutadahili ngazi
ya cheti kama ilivyokuwa zamani," amesema Dk Msonde.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni