Jumatano, 23 Novemba 2016

MADEREVA WANAOACHA MAWE NA MAGOGO BARABARANI KUKAMATWA.



WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba ameziagiza mamlaka zinazohusika kuwadhibiti madereva wanaoacha ovyo mawe barabarani baada ya kumaliza kufanya matengenezo ya magari yao.

Mwigulu ametoa agizo hilo jana wakati wa kikao cha 38 cha Bodi ya Barabara Mkoa wa Singida kilichofanyika mjini Singida.

Alisema kwa muda mrefu sasa baadhi ya madereva hasa wa magari makubwa, wamekuwa wakifanya matengenezo ndani ya maeneo ya barabara na kutumia mawe makubwa kuzuia magari yao yasirudi nyuma.

"Ukiharibikiwa na gari barabarani hakikisha unaondoa mawe yote uliyoweka hapo kabla ya kuondoka ili kuepusha ajali zisizo za lazima. Unaacha mawe barabarani nani aje ayaondoe? Naagiza mamlaka zinazohusika kuanzia sasa ziwakamate madereva wote wa aina hiyo na kuwarejesha walikoacha hayo mawe, waende kuyaondoa hata kama ni mbali kiasi gani ili iwe ni fundisho kwa wengine," ameagiza.

Amekemea tabia ya baadhi ya wananchi wenye mazoea ya kupitisha au kuswaga mifugo yao barabarani na kusema kuwa licha ya kitendo hicho kuweza kusababisha ajali, pia huharibu barabara zinazojengwa kwa gharama kubwa.

Mwigulu ambaye pia ni Mbunge wa Iramba Magharibi mkoani hapa alitoa rai kwa viongozi wa ngazi zote nchini kuhakikisha wanatoa elimu ya kutosha kwa jamii juu ya matumizi bora ya barabara zote.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni