JESHI la Polisi nchini, katika kuhakikisha usalama wa raia
na mali zao unaimarika, limeendelea na operesheni za kukamata wahalifu wa
makosa mbalimbali yakiwemo makosa ya usalama barabarani katika mikoa yote ili
kudhibiti vitendo vya uhalifu na wahalifu.
Katika operesheni hizo, Jeshi la Polisi limefanikiwa
kukamata silaha na katika baadhi ya mikoa, wananchi wameweza kusalimisha silaha
kwa hiari katika vituo vya Polisi.
Operesheni hizi ni endelevu, na ili tuweze kufanikiwa zaidi
katika kudhibiti uhalifu na wahalifu hususani katika kipindi hiki tunapoelekea
mwisho wa mwaka, wananchi wanatakiwa kuwa makini na kutoa taarifa za uhalifu na
wahalifu haraka kwa kutumia namba za bure 111 na 112 pindi wanapowatilia shaka
watu wasiowajua katika maeneo yao ili hatua za haraka ziweze kuchukuliwa.
Kwa wamiliki wa maduka makubwa, hoteli na maduka ya kufanyia
miamala ya fedha kwa njia ya simu waangalie namna ya kuweka vifaa maalumu
vyenye uwezo wa kurekodi mienendo ya watu wanaoingia na kutoka ama kufuata
huduma katika maeneo yao ya biashara.
Pia, wananchi katika makazi yao waimarishe ulinzi kwa
kutumia mpango wa ulinzi jirani kwa kuhakikisha wanakuwa na utaratibu wa
kubadilishana taarifa za hali ya usalama ili kuhakikisha mitaa yao inakuwa
salama wakati wote.
Aidha, Jeshi la Polisi nchini linawataka madereva wa vyombo
vya moto kuheshimu na kutii sheria za usalama barabarani ili kuepusha ajali na
kuokoa maisha ya abiria na watumiaji wengine wa barabara.
Jeshi la polisi nchini, litaendelea kutekeleza majukumu yake
kwa mujibu wa sheria, bila woga ama upendeleo katika kuhakikisha usalama wa
raia na mali zao unaimarika.
Imetolewa
na:
Advera
John Bulimba - Kamishina Msaidizi wa Polisi (ACP)
Msemaji
wa Jeshi la Polisi,
Makao
Makuu ya Polisi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni