Akizungumza nyumbani kwa marehemu, Meya wa Kinondoni,
Benjamini Sitta ambaye ni mtoto wa kiume wa marehemu, alisema kuwa baba yake
alitoa maneno matatu ya kuukubali ukweli wa maisha baada ya Daktari kumueleza
kuwa asingeweza kupona.
“That’s life (hayo ndiyo maisha),” Benjamin alikariri maneno ya baba yake. Alisema hayo
yalikuwa maneno yake ya mwisho baada ya kuelezwa ukweli na daktari wa hospitali
ya Technical University of Munich nchini Ujerumani alipokuwa akipatiwa
matibabu.
Maneo ya Sitta ni funzo kubwa kwa watu wote kuwa maisha
huanza na huisha, hiyo ndiyo maana ya maisha na hakuna aishie milele hivyo
tuishi kwa kuzingatia maana hiyo ya maisha na kuikubali.
Sitta ambaye anakumbukwa kwa kauli mbiu yake na matendo ya
kusimamia ‘kasi na viwango’, alifariki kutokana na ugonjwa wa tezi dume
uliokuwa ukimsumbua kwa muda mrefu.
Alitangaza kustaafu siasa muda mfupi baada ya kukamilika kwa
kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka jana, ambapo yeye alikuwa mmoja kati ya
waliokuwa msitari wa mbele kumnadi mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi, Dkt.
John Magufuli aliyeshinda uchaguzi huo.
Benjamini alieleza kuwa marehemu atazikwa Urambo Mkoani
Tabora na kwamba ratiba ya mazishi itatolewa na Ofisi ya Bunge ambayo ndiyo
inayoratibu mazishi
“Tumempoteza
baba na kiongozi ambaye tulikuwa tunamtegemea kwa ushauri na masuala
mbalimbali, tutafuata yale aliyokuwa akituelekeza,” alisema Benjamini.
Rais Dkt. John Pombe Magufuli alifika kumjulia hali mzee Sitta enzi za uhai wake alipolazwa katika hospitali ya Muhimbili jijini Dar es salaam.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni