SERIKALI ya awamu ya Tano inayoongozwa na Dkt. John
Pombe Magufuli imepongezwa kwa juhudi inazochukua katika kutatua changamoto
mbalimbali zinazowakabili wananchi.
Kauli hiyo imetolewa leo Jijini Dar es salaam na
Msaidizi wa Askofu wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani ya Kanisa la Kiinjili la
Kilutheri Tanzania (KKKT) Mchungaji Chediel Luiza wakati wa Ibada ya
kuaga mwili wa Spika Mstaafu Marehemu Mhe. Samweli Sitta.
“Viongozi wetu wa sasa wametambua kuwa jamii yetu
inakabiliwa na changamoto mbalimbali na wameanza kuchukua hatua za makusudi”
alisisitiza mchungaji Luiza.
Akifafanua zaidi Mchungaji Luiza amesema ni muhimu
kwa kila mtu kutumia nafasi yake kuwatumikia wananchi kwa uadilifu na kwa
maslahi mapana ya Taifa kama alivyofanya Marehemu Samweli Sitta.
“Hatua yakuwatumikia wananchi wa uadilifu na
uzalendo ilimjengea heshima kubwa Mhe. Samweli Sitta katika kipindi chote cha
uhai wake” alisema Mchngaji Luiza.
Kwa upande wake msemaji wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)
Christopher Ole Sendeka amesema kuwa Marehemu alifanikisha mabadiliko makubwa
katika Bunge la 9 akiwa Spika ikiwemo kuanzishwa kwa Mfuko wa jimbo ili
kuchochea maendeleo katika majimbo yote hapa nchini.
“Alipambana kupiga vita rushwa na vitendo vyote vya
ufisadi katika kipindi chote cha uhai wake kwa maslahi mapana ya wananchi wa
Tanzania”alisisitiza Olesendeka.
Aidha ameongeza kuwa Marehemu Sitta alichangia
kuinua hadhi ya Kituo cha uwekezaji Tanzania (TIC) na kuwa moja ya vituo bora
vya uwekezaji Barani Afrika.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni