WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame
Mbarawa ametoa muda wa mwezi mmoja kwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Ndege
Tanzania (ATCL), kufanya mabadiliko katika menejimenti ya Shirika hilo ili
kuongeza ufanisi na kuboresha utendaji kazi.
Ametoa agizo hilo jijini Dar es Salaam alipokuwa akizungumza
katika mkutano wa Menejimenti pamoja na wafanyakazi wa Shirika hilo na kuwataka
kutoa huduma bora ili kulifanya Shirika hilo kuwa miongoni mwa mashirika bora
ya ndege barani Afrika.
“Nataka ndani ya mwezi mmoja uwe
umeshafanya mabadiliko katika menejimenti, mabadiliko lazima yaanzie juu kwanza
kwa watoa maamuzi na ishuke hadi kwa wafanyakazi wazembe na wasio waadilifu,” amesema Waziri Prof. Mbarawa.
Waziri Mbarawa amepinga nyongeza ya mshahara kwa wafanyakazi
wa Shirika hilo hasa katika kipindi hiki ambacho Serikali ipo katika juhudi za
kulifufua na kuliimarisha Shirika hilo.
Aidha Waziri Mbarawa ameitaka Idara ya Masoko ya shirika
hilo kuzunguka katika taasisi zote zilizo chini ya Wizara yake na kuzishawishi
kuweza kutumia huduma za usafiri wa anga wa ATCL.
“Serikali imekamilisha upande
wake wa ununuzi wa ndege, sasa kazi inabaki kwenu, sitaki watu wa masoko kukaa
ofisini”, amesema Prof. Mbarawa.
Ameongeza kuwa wafanyakazi wa ATC wanatakiwa kujipanga kutoa
huduma iliyotukuka kwa wateja wake ili kuweza kuhimili ushindani uliopo katika
mashirika ya ndege nchini.
“Inabidi tofauti kubwa ionekane
kati yenu na mashirika mengine, yeyote ambaye anaona hawezi kutoa huduma bora
kwa mteja atafute sehemu nyingine kwani hapa hatufai ”, amesisitiza Waziri Mbarawa.
Profesa Mbarawa amelitaka shirika hilo kutumia mfumo wa
kisasa wa kukata tiketi kwa njia ya simu na kompyuta ili kuwarahishia watumiaji
wa shirika hilo kuweza kupata tiketi kwa haraka na urahisi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo Eng.
Ladislaus Matindi amemhakikishia Waziri Mbarawa kufanyia kazi maagizo aliyotoa
na kuahidi kuboresha utendaji kazi wa shirika hilo kwa lengo la kuteka soko la
ushindani wa usafiri wa anga nchini.
“Kwa sasa tumeanza vizuri na
naamini uwezo wa kuzalisha faida zaidi tunao, tunaahidi kuboresha utendaji kazi
ili kuendana na kasi ya mabadiliko ya Serikali ya Awamu ya Tano,” amesema Eng. Matindi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni