WATUMISHI wa Umma 1,663 kutoka Wizara, Idara
zinazojitegemea, Wakala za Serikali, Sekretarieti za Mikoa, na Mamlaka za
Serikali za Mitaa wamechukuliwa hatua za kinidhamu baada ya kubainika
kusababisha watumishi hewa 19,629 hadi Oktoba 25, 2016.
Waziri ya Nchi, Ofisi ya Rais, anayeshughulikia Utumishi na
Utawala Bora Angella Kairuki amesema hayo jana Bungeni mjini Dodoma alipokuwa
akijibu swali la Mainda Hamad Abdallah (Mbunge wa Viti Maalum) alilohoji hatua zilizochukuliwa
na Serikali dhidi ya watumishi waonarudisha nyuma maendeleo ya nchi.
Akifafanua idadi hiyo, Waziri Kairuki alisema kuwa idadi ya
watumishi waliochukuliwa hatua za kinidhamu kutoka Wizara mbalimbali ni 16,
Idara zinazijitegemea na Wakala za Serikali watumishi tisa, Sekretarieti za
Mikoa watumishi sita na Mamlaka za Serikali za Mitaa watumishi 1,632.
Waziri Kairuki alisema kuwa watumishi hao wameisabishia
Serikali hasara ya zaidi ya Sh. bilioni 19, huku Halmashauri ya Kinondoni ikiwa
na watumishi hewa 107 ambao waligharimu Serikali sh. bilioni 1.29, Kishapu
watumishi 73 wamesababisha hasara ya kwa kugharimu sh. milioni 543 na kuonya
kuwa waajiri waendelee kuchukua hatua za haraka na kudhibiti uwepo wa watumishi
hewa ili kuipunguzia Serikali kuingia hasara kubwa badala ya kuwahudumia
wananchi.
Aidha, Waziri Kairuki alisema kuwa jumla ya watumishi 638
wamefunguliwa mashtaka polisi, watumishi 50 wanafanyiwa uchunguzi na Taasisi ya
Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) na watumishi 975 mashtaka yao
yamefikishwa kwenye Mamlaka zao za kinidhamu.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni