Alhamisi, 24 Novemba 2016

SHIRIKISHO LA VYAMA VYA WAFANYAKAZI TANZANIA (TUCTA) YALIA NA TIMUA TIMUA.

 SHIRIKISHO la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta) wametoa kilio chao kwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakielezwa kukerwa na tabia ya wakuu wa mikoa, wilaya na wakurugenzi wanaowaweka ndani kiholela, kuwanyanyasa wafanyakazi na kuwashusha vyeo.

Lakini Waziri Mkuu Majaliwa amesisitiza kuwa serikali haitawafumbia macho watumishi wasio waadilifu na wasiofuata taratibu za kazi, akisema “tutaendelea kuchukua hatua kali kwa mujibu wa sheria na taratibu.”

Akisoma risala katika Mkutano Mkuu wa Sita wa Tucta mbele ya Waziri Mkuu jana mjini hapa, Katibu Mkuu wa Tucta, Nicholaus Mgaya alisema hivi karibuni kumeibuka tabia ya baadhi ya wanasiasa wakiwemo wakuu wa mikoa, wilaya na wakurugenzi wakihusika na vitendo vya kuwaweka ndani, kuwanyanyasa, kuwashusha vyeo na hata kuwasimamisha kazi watumishi walio chini yao bila ya kufuata taratibu zilizowekwa kisheria.

Mgaya alisema jambo hilo hawalikubali kwa nguvu zote kwani limekuwa likifanywa bila ya kufuata kanuni na taratibu za utumishi wa umma.

“Sisi kama viongozi wa vyama vya wafanyakazi hatukubali jinsi wanasiasa wanavyowafukuza kazi watumishi kwa kutaka mambo yao yaende vizuri. Tungependa kuona sheria zinafuatwa pale ambapo masuala ya nidhamu ya mfanyakazi yanahusika ili kuondoa maonevu yasiyokuwa ya lazima. Waswahili husema mnyonge mnyongeni, lakini haki yake mmpe,” alisema Mgaya huku akishangiliwa na wajumbe mkutano huo.

Akijibu suala hilo, Waziri Mkuu Majaliwa alisema serikali ya Rais John Magufuli itaendelea kuzingatia utawala wa sheria na kanuni za utawala bora ili kuhakikisha kuwa haki za wafanyakazi nchini zinalindwa ipasavyo.

Majaliwa aliwaagiza viongozi wa kisiasa nchini katika wizara mbalimbali, mikoa, wilaya, idara za serikali, halmashauri na taasisi zote za serikali kuzingatia utawala wa sheria katika kushughulikia masuala mbalimbali yanayohusu wajibu na haki za wafanyakazi.

Pia alitoa rai kwa wafanyakazi wote nchini kutekeleza majukumu yao kwa nidhamu, uwajibikaji na uadilifu katika maeneo yao ya kazi “Ni dhahiri nidhamu ya kazi imeporomoka kidogo kutokana na watumishi kutotimiza wajibu wao na wengine ni wabadhirifu wa mali za serikali, serikali haitawafumbia macho, tutaendelea kuchukua hatua kali kwa mujibu wa sheria na taratibu,” alisisitiza Waziri Mkuu.

Pia katika risala hiyo, wafanyakazi hao walimlilia Waziri Mkuu wakimwomba wakutane na Rais Magufuli ili wazungumza naye kuhusu matatizo yao.

“Mheshimiwa Waziri Mkuu awamu zilizopita za uongozi wa vyama vya wafanyakazi zimekuwa zikipewa nafasi ya kuonana na Rais, kwetu imekuwa tofauti tulitakiwa tuonane naye Mei Mosi 2016, lakini haikuwezekana tulijulishwa mara atakapopata nafasi tutaitwa, ombi letu kwetu kwako tunaomba kuonana naye,” alisema Katibu Mkuu wa Tucta.

Pia alizungumzia suala la wafanyakazi kuajiriwa bila ya mikataba ya ajira limekuwa ni suala sugu na hata waajiri wengi wamekuwa wakitembelewa na maofisa kazi kuhusu hilo, lakini wamekuwa wajeuri na kuendelea kuajiri bila ya kuwapa mikataba.

Alisema kukosekana kwa kanuni za uandikishwaji wa vyama vya wafanyakazi, waajiri limekuwa ni tatizo kubwa kwao kutokana na kuandikishwa kiholela wa vyama wafanyakazi na hata kukwepo kwa vyama vya wafanyakazi mfukoni visivyokuwa na ofisi wala anuani.

“Waziri Mkuu imekuwa ni jambo la kawaida kwa watumishi wa umma kutopandishwa vyeo kwa muda mrefu bila sababu yoyote na wengine kunyimwa nyongeza zao za mishahara kila mwaka, wapo watumishi wamekaa katika ngazi moja kwa zaidi ya miaka kumi,” alieleza Mgaya.

Akizungumzia mikataba ya ajira kwa wafanyakazi, Waziri Mkuu Majaliwa alitoa maagizo kwa waajiri wote nchini kutoa mikataba hiyo mara moja kwa wafanyakazi wao, na kuwaagiza maofisa wa kazi nchini kuhakikisha kila mwajiri anafikiwa na hatua stahiki na amezijua ili kumpa mwajiriwa wake.

“Kifungo cha 14 cha Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini Namba 6 ya Mwaka 2004 kinaeleza aina ya mbalimbali za mikataba inayotakiwa kutumika katika kuajiri wafanyakazi,” alieleza Waziri Mkuu.

Awali akitoa salamu kutoka Kenya, Katibu wa Shirikisho la Wafanyakazi Kenya (Cotu), Francis Atwoli aliomba wananchi wa Tanzania wawapatie Dk Magufuli ili akawanyooshe wafanyakazi wa nchini mwao.

“Muungeni mkono Rais Magufuli, badala ya kulalamika kuwa kasi yake ni kubwa mno, Tunaendelea kumuunga mkono Rais Magufuli na msipomtumia hebu tukopesheni mwaka mmoja ili akatunyooshee wafanyakazi wa Kenya,” alieleza Atwoli na kushangiliwa na wajumbe wa mkutano huo ambao leo utawachagua viongozi wa Tucta watakaoiongoza kwa miaka mitano ijayo.



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni