Jumatatu, 28 Novemba 2016

WANAWAKE NCHINI WAMETAKIA KUJITAMBUA, KUJIAMINI NA SIMAMIA HAKI ZAO IKIWA NI KAULI MBIU YA SIKU 16 ZA KUPINGA UKATILI WA KIJINSIA .



WANAWAKE wa kitanzania wametakiwa kupigania haki zao bila kujali vikwazo wanavyokutana navyo katika mchakato wa kukabiliana na ukatili wa kijinsia katika kada zote, huku wakisaidiana na kujiamini katika kufikia lengo lao la kuhakikisha haki za wanawake zinasimamiwa.

Hayo yamesemwa na spika mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Anne Makinda, jijini Dar es salaam wakati akifungua kongamano la kwanza la kitaifa la haki za wanawake.

Mhe. Makinda alisema wanawake waache kuwa nyuma badala yake wasimame kuzipigania haki zao na kuhakikisha kuwa malengo ya kumkomboa mwanamke yanafikiwa bila kukatishwa tama, hata mimi nisingesimama mwenyewe nisingeweza kufikia nafasi nilizozifikia ikiwemo mfumo dume unao zaa unyanyasaji wa kijinsia.

Mhe, Makinda pia aliitaka serikali kuweka mikakati ya namna ya kusaidia mashirika yasiyo ya kiserikali yanayojihusisha na kutetea haki za wanawake nchini badala ya kutegemea wahisani pekee kwakuwa wao hufanya hivyo kwa kipindi maalum na baada ya hapo mashirika hayo hubaki bila msaada.

Kongamano hilo limeandaliwa na mfumo wa msaada wa kisheria (LSF) na kushirikisha wadau mbalimbali wa kutetea haki za wanawake nchini na kauli mbiu katika kongamano hilo ni “Jitambue, Jiamini,Simamia haki yako”

Akizungumza kwenye kongamano hilo, afisa  mtendaji mkuu wa LSF, Kess Greonerndijk, alisema wameamua kusaidia mapambano dhidi ya ukatili kwa wanawake na kusimamia haki zao kwakuwa bado kuna uhitaji mkubwa wa kufanya hivyo kutokana na matukio mengi ya kikatili yanayo ripotiwa kufanywa dhidi ya wanawake


HALMASHAURI YA WILAYA YA HANDENI YAFANIKIWA KUTEKELEZA AGIZO LA RAIS JOHN POMBE MAGUFULI.

MAPATO yatokanayo na makusanyo ya ndani katika Halmashauri ya wilaya ya Handeni yameongezeka mara dufu kutoka sh. Milioni 25 hadi milioni52 kwa mwezi baada ya uongozi kuacha kutumia mawakala kuanzia Septemba mosi mwaka huu.

Hatua hiyo imefikiwa ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania John Pombe Magufuli  la kuzitaka halmashauri zote nchini kubadili utaratibu kwa kuacha kutumia mawakala na kuanza mara moja kukusanya zenyewe mapato yake kutoka kwenye vyanzo mbalimbali vya ndani.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Handeni, William
Makufwe amebainisha hayo jana mjini humo katika mahojiano na Mwandishi wetu kuhusu utekelezaji wa maagizo mbalimbali ya serikali ikiwemo suala la kuongeza wigo wa ukusanyaji mapato.

“Nakumbuka moja ya mambo tuliyoagizwa na rais mara baada ya uteuzi ni
kuongeza wigo wa ukusanyaji mapato na mwenyewe (rais) alisisitiza
kwamba ni vizuri halmashauri zikakusanya zenyewe badala ya kutumia
mawakala ambao kwa kiasi kikubwa walikuwa wakiziibia halmashauri, ...
hivyo niliamua kuandaa mkakati maalum wa kuwatumia viongozi na
watendaji ngazi ya kata na vijiji kukusanya badala ya mawakala,”
alisema na kuongeza.

“Tulianza utekelezaji Septemba mosi mwaka huu kwa kuwahusisha
madiwani, wenyeviti wa serikali za vijiji pamoja na watendaji wa idara
zote kwenye kata na vijiji ambao jukumu lao ni kusimamia wenyewe
ukusanyaji mapato katika maeneo yao,”alisema.

Aidha, Makufwe alisema ukusanyaji mapato huo umehusisha matumizi ya
mashine 30 za utoaji risisti za kielektroniki ili kurahisisha na
kudhibiti makusanyo ambayo yanatarajiwa kuiongezea halmashauri uhakika
wa fedha badala ya kutegemea kwa kiasi kikibwa ruzuku ya serikali.

“Ki msingi kabla ya mkakati wetu huu kuanza kutekelezwa halmashauri
ilikuwa ikikusanya kupitia mawakala wake kiasi cha sh. Milioni 25 kwa
mwezi lakini kati ya Septemba mosi hadi 30 mwaka huu makusanyo
yameongezeka na kufikia sh. Milioni 52,matarajio yangu ni kufikia
makusanyo ya wastani wa kati y ash. Milioni 90 hadi 100 msimu kama huu
mwakani,”alisema.

Hata hivyo, ametaja changamoto kubwa katika utekelezaji wa mkakati huo
kwa sasa ni ukosefu wa uaminifu na uadilifu miongoni mwa baadhi ya
watendaji na viongozi wanaosimamia jukumu hilo na kusisitiza kwamba
watashughulikia.


Alhamisi, 24 Novemba 2016

SHIRIKISHO LA VYAMA VYA WAFANYAKAZI TANZANIA (TUCTA) YALIA NA TIMUA TIMUA.

 SHIRIKISHO la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta) wametoa kilio chao kwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakielezwa kukerwa na tabia ya wakuu wa mikoa, wilaya na wakurugenzi wanaowaweka ndani kiholela, kuwanyanyasa wafanyakazi na kuwashusha vyeo.

Lakini Waziri Mkuu Majaliwa amesisitiza kuwa serikali haitawafumbia macho watumishi wasio waadilifu na wasiofuata taratibu za kazi, akisema “tutaendelea kuchukua hatua kali kwa mujibu wa sheria na taratibu.”

Akisoma risala katika Mkutano Mkuu wa Sita wa Tucta mbele ya Waziri Mkuu jana mjini hapa, Katibu Mkuu wa Tucta, Nicholaus Mgaya alisema hivi karibuni kumeibuka tabia ya baadhi ya wanasiasa wakiwemo wakuu wa mikoa, wilaya na wakurugenzi wakihusika na vitendo vya kuwaweka ndani, kuwanyanyasa, kuwashusha vyeo na hata kuwasimamisha kazi watumishi walio chini yao bila ya kufuata taratibu zilizowekwa kisheria.

Mgaya alisema jambo hilo hawalikubali kwa nguvu zote kwani limekuwa likifanywa bila ya kufuata kanuni na taratibu za utumishi wa umma.

“Sisi kama viongozi wa vyama vya wafanyakazi hatukubali jinsi wanasiasa wanavyowafukuza kazi watumishi kwa kutaka mambo yao yaende vizuri. Tungependa kuona sheria zinafuatwa pale ambapo masuala ya nidhamu ya mfanyakazi yanahusika ili kuondoa maonevu yasiyokuwa ya lazima. Waswahili husema mnyonge mnyongeni, lakini haki yake mmpe,” alisema Mgaya huku akishangiliwa na wajumbe mkutano huo.

Akijibu suala hilo, Waziri Mkuu Majaliwa alisema serikali ya Rais John Magufuli itaendelea kuzingatia utawala wa sheria na kanuni za utawala bora ili kuhakikisha kuwa haki za wafanyakazi nchini zinalindwa ipasavyo.

Majaliwa aliwaagiza viongozi wa kisiasa nchini katika wizara mbalimbali, mikoa, wilaya, idara za serikali, halmashauri na taasisi zote za serikali kuzingatia utawala wa sheria katika kushughulikia masuala mbalimbali yanayohusu wajibu na haki za wafanyakazi.

Pia alitoa rai kwa wafanyakazi wote nchini kutekeleza majukumu yao kwa nidhamu, uwajibikaji na uadilifu katika maeneo yao ya kazi “Ni dhahiri nidhamu ya kazi imeporomoka kidogo kutokana na watumishi kutotimiza wajibu wao na wengine ni wabadhirifu wa mali za serikali, serikali haitawafumbia macho, tutaendelea kuchukua hatua kali kwa mujibu wa sheria na taratibu,” alisisitiza Waziri Mkuu.

Pia katika risala hiyo, wafanyakazi hao walimlilia Waziri Mkuu wakimwomba wakutane na Rais Magufuli ili wazungumza naye kuhusu matatizo yao.

“Mheshimiwa Waziri Mkuu awamu zilizopita za uongozi wa vyama vya wafanyakazi zimekuwa zikipewa nafasi ya kuonana na Rais, kwetu imekuwa tofauti tulitakiwa tuonane naye Mei Mosi 2016, lakini haikuwezekana tulijulishwa mara atakapopata nafasi tutaitwa, ombi letu kwetu kwako tunaomba kuonana naye,” alisema Katibu Mkuu wa Tucta.

Pia alizungumzia suala la wafanyakazi kuajiriwa bila ya mikataba ya ajira limekuwa ni suala sugu na hata waajiri wengi wamekuwa wakitembelewa na maofisa kazi kuhusu hilo, lakini wamekuwa wajeuri na kuendelea kuajiri bila ya kuwapa mikataba.

Alisema kukosekana kwa kanuni za uandikishwaji wa vyama vya wafanyakazi, waajiri limekuwa ni tatizo kubwa kwao kutokana na kuandikishwa kiholela wa vyama wafanyakazi na hata kukwepo kwa vyama vya wafanyakazi mfukoni visivyokuwa na ofisi wala anuani.

“Waziri Mkuu imekuwa ni jambo la kawaida kwa watumishi wa umma kutopandishwa vyeo kwa muda mrefu bila sababu yoyote na wengine kunyimwa nyongeza zao za mishahara kila mwaka, wapo watumishi wamekaa katika ngazi moja kwa zaidi ya miaka kumi,” alieleza Mgaya.

Akizungumzia mikataba ya ajira kwa wafanyakazi, Waziri Mkuu Majaliwa alitoa maagizo kwa waajiri wote nchini kutoa mikataba hiyo mara moja kwa wafanyakazi wao, na kuwaagiza maofisa wa kazi nchini kuhakikisha kila mwajiri anafikiwa na hatua stahiki na amezijua ili kumpa mwajiriwa wake.

“Kifungo cha 14 cha Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini Namba 6 ya Mwaka 2004 kinaeleza aina ya mbalimbali za mikataba inayotakiwa kutumika katika kuajiri wafanyakazi,” alieleza Waziri Mkuu.

Awali akitoa salamu kutoka Kenya, Katibu wa Shirikisho la Wafanyakazi Kenya (Cotu), Francis Atwoli aliomba wananchi wa Tanzania wawapatie Dk Magufuli ili akawanyooshe wafanyakazi wa nchini mwao.

“Muungeni mkono Rais Magufuli, badala ya kulalamika kuwa kasi yake ni kubwa mno, Tunaendelea kumuunga mkono Rais Magufuli na msipomtumia hebu tukopesheni mwaka mmoja ili akatunyooshee wafanyakazi wa Kenya,” alieleza Atwoli na kushangiliwa na wajumbe wa mkutano huo ambao leo utawachagua viongozi wa Tucta watakaoiongoza kwa miaka mitano ijayo.



Jumatano, 23 Novemba 2016

AFYA YA MKUU WA MKOA WA TANGA YATENGEMAA.



WAZIRI wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Nape Moses Nnauye amefika katika hospitali ya Muhimbili kumjulia hali Mkuu wa Mkoa wa Tanga Martin Shigela aliyelazwa katika wodi ya Sewahaji Jijini Dar es Salaam.

Kwa taarifa zilizopo hali ya Mkuu wa mkoa wa Tanga Shigela kwa sasa anaendelea vizuri.

Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini WHUSM

NAIBU WAZIRI WA OFISI YA RAIS TAWALA NA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA TAMISEMI SULEIMAN JAFFO AFANYA ZIARA WILAYANI PANGANI MKOANI TANGA.


SERIKALI ipo kwenye mpango wa  kuanza utekelezaji wa ujenzi wa vituo vya afya katika kila kata nchi mzima ili kumaliza changamoto ya upungufu huo uliopo kwa sasa katika maeneo mengi.

Rai hiyo ilitolewa na Naibu Waziri wa ofisi ya Rais Tawala na mikoa na serikali za mitaa TAMISEMI Suleiman Jaffo wakati wa ziara yake wilayani Pangani.

Alisema mpango huo unatarajiwa kuanza utekelezaji wake kuanzia mwaka ujao wa fedha kwa kila Halimashauri kujengewa kituo kimoja cha afya katika ngazi yakata .

Pia alisema kupitia mpango huo serikali itaweza kwa kiasi fulani kufikia lengo la lake iliyojiwekea la kila kata kuwa na kituo cha afya ili kusogeza huduma karibu na wananchi.

Aidha Naibu Waziri huyo alisema kuwa licha ya utekelezaji wa Sera ya afya kutiliwa mkazo katika maeneo mengi hapa nchini bado  mpaka sasa Tanzania mzima inavituo vya afya 440 pekee.

Kwa Upande wake Mkuu wa Wilaya ya Pangani Zainab Abdallah alisema kuwa wilaya hiyo inakata 14 lakini ina kituo cha afya kimoja hali inayosababisha changamoto ya utoaji wa huduma.


Wilaya yetu maeneo kata nyingine zimetenganishwa na mto Pangani hivyo kutoka na hali hiyo tumelazimika kujenga kituo cha afya katika kata za ngambo ili tuweze kuwahudumia wananchi wote" alisema Dc huyo.