Jumanne, 4 Oktoba 2016

WIKI YA MAADHIMISHO YA AFYA YA AKILI WANANCHI WATAKIWA KUPUNGUZA MSONGO UNAOSABABAISHA MATATIZO YA AKILI







Afisa afya tiba ya akili mkoa wa Tanga Dokta Wallece Karata akiwaelimisha waandishi wa habari ambao hawapo kwenye picha kupambana na msongo wa mawazo. 

HABARI.



·       Msongo wa mawazo watajwa kuwa chanzo cha ongezeko la watu wenye upungufu wa akili hii nikutokana na waliowengi kuvumilia maumivu wanayokutana nayo kwenye ndoa ,uhusiano wa mapenzi na magonjwa ya muda mrefu katika miili ya wanadamu na hata katika kazi zetu za kuajiriwa.

Hayo ameyasema mratibu wa afya ya akili wa mkoa wa Tanga Anitha Temu alipoongea na waandishi wa habari katika ukumbi wa RODASACK uliopo Hospitali ya rufaa Bombo katika kufungua  maadhimisho ya wiki ya afya ya akili katika mkoa wa tanga.

Siku hii ya afya ya akili inaadhimishwa duniani kote kila mwaka oktoba 10 na maadhimisho haya kitaifa yatafanyika wilaya ya Korogwe Mkoani hapa kwa kutembelea hospitali ya Magunga na hospitali ya watu wenye upungufu wa akili Lutindi.

Mratibu afya ya akili Anitha Temu hakusita kutaja idadi ya watu walioathiwa na madawa ya kulevya katika mkoa huu wa Tanga na kusema idadi ya wanaume kwa mwaka 2015-2016 ni mia saba ishirini na nane(728) na wanawake ni kumi na moja (11)huku wanaume wakiongoza kwa kuwa na idadi kubwa na hawa ni wale waliojitokeza katika vituo viwili vya soba vilivyopo mkoani hapa.
 
Pia  Mratibu afya akili Temu  alisema changamoto wanayokutana nayo katika hospitali ya mkoa Bombo ikiwa pamoja na kukosa nyumba ya kuwahifadhi ama kuwalaza wagonjwa wa akili pindi waletwapo kupata matibabu na kulazimika kuwachanganya na wagonjwa wengine kitendo ambacho ni hatarishi kwa wagonjwa wengine.

Alisema kwa sasa wanalazimika kuwapa dawa za usingizi baadhi ya wagonjwa hao wa akili ili kuepusha usumbufu kwa wagonjwa wengine wa kawaida.

Hata hivyo alisema wapo katika mchakato wa kukarabati jengo maalumu la wagonjwa wa akili katika hospitali ya mkoa Bombo na ifikapo januari 2017 jengo hilo litakuwa limekamilika.

Nae afisa afya tiba ya akili dokta Wallece Karata amesema katika majaribio ya kujiuwa wanawake ni wengi wanaojaribu kujiuwa lakini wanafanikiwa kuokolewa wakati kwa wanaume ni wachache wanaojaribu kujiuwa na wanafanikiwa kutokana na uwamuzi wao mgumu wa kutoishirikisha jamii.

Mratibu wa afya ya aikili mkoa Anitha Temu ametoa wito kwa wananchi wa mkoa wa tanga kwa wale wenye msongo wa mawazo ama wa kisaikolojia ambao wameathirika ndani ya nafsi zao waweze kufika hospitalini hapo ili kupata ushauri zaidi na sio kujichukulia maamuzi ya kujiua sio suluhisho la kumaliza matatizo.

KAULI MBIU:” UTU KATIKA AFYA YA AKILI HUDUMA ZA KISAIKOLOJIA NA AFYA YA AKILI KUWA HUDUMA YA KWANZA KWA WOTE”
 


 





Hakuna maoni:

Chapisha Maoni