RAIS wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) Mhe. Joseph
Kabila Kabange, amewasili hapa nchini jana tarehe 03 Oktoba, 2016 kwa ziara
rasmi ya kiserikali ya siku tatu na kupokelewa na mwenyeji wake Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli.
Pamoja na Rais Magufuli viongozi wengine waliompokea Rais
Joseph Kabila Kabange ni Makamu wa Rais Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Wakuu
wa vyombo vya ulinzi na usalama, viongozi mbalimbali wa Serikali, Mabalozi na
wananchi.
Katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere Jijini
Dar es Salaam, Rais Joseph Kabila Kabange alipokea heshima ya kupigiwa mizinga
21 na kukagua gwaride rasmi lililoandaliwa kwa ajili yake na baadaye kushuhudia
burudani ya vikundi vya ngoma.
Leo tarehe 04 Oktoba, 2016 Rais Joseph Kabila Kabange
atafanya mazungumzo rasmi na mwenyeji wake Rais John Pombe Magufuli, ataweka
jiwe la msingi la jengo la Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) na baadaye
kushiriki dhifa ya kitaifa iliyoandaliwa na Mwenyeji wake Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa pamoja na mgeni wake wake Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Joseph Kabila wakati nyimbo za Taifa za mataifa yote mawili zikipigwa kabla ya ukaguzi wa gwaride lililoandaliwa kwa ajili ya heshima yake.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni