Alhamisi, 27 Oktoba 2016

MFANYABIASHARA MAARUFU ARUSHA KIZIMBANI KWA KUMNAJISI MTOTO WA KUMZAA.

Mfanyabiashara maarufu jijini Arusha na mkazi wa kata ya Sakina, Alistalius Silayo (45) amefikishwa mahakamani akituhumiwa kumnajisi mtoto wake wa kumzaa mwenye umri wa miaka 11.

Akisomewa mashitaka na Mwendesha Mashitaka wa Serikali, Pennina Joackim ilidai kuwa mfanyabiashara huyo alitenda kosa hilo katika vipindi tofauti kati ya Januari na Septemba mwaka huu.

Mwendesha Mashitaka alidai mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya Arusha, Patricia Kisinda kuwa mshtakiwa alikuwa akifanya kosa hilo mara kwa mara katika miezi hiyo eneo la Sakina kwa Iddy yaliko makazi yake.

Alidai mshtakiwa alitenda kosa hilo kinyume cha Kifungu cha 158 Kifungu kidogo cha 1(a) cha Sheria na Kanuni ya Adhabu Sura ya 16 na kufanyiwa marekebisho 2002.

Baada ya kusomewa mashitaka, mshitakiwa alikana shitaka hilo na hakimu alisema dhamana iko wazi ya wadhamini wawili wanaotambulika kisheria. 
Mbali ya hilo, pia wadhamini hao lazima wawe na mali isiyohamishika yenye thamani ya zaidi Sh milioni 10 na wadhamini hawaruhusiwi kutoka nje ya Mkoa wa Arusha bila ya kibali cha Mahakama.

Hata hivyo, wadhamini hao walishindwa kukamilisha taratibu za dhamana mahakamani hapo na hakimu aliwapa muda kukamilisha taratibu katika saa za kazi na kuamuru mshtakiwa kurudishwa rumande hadi taratibu zitakapokamilika. 
Kesi hiyo itatajwa tena Novemba 10, mwaka huu kwani Mwanasheria wa Serikali alidai upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni