Ijumaa, 27 Januari 2017

SHEREHE YA SIKU YA SHERIA KUANZA RASMI KESHO MKOANI TANGA.

JAJI Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Tanga, Mhe. Imani Aboud amesema yapo mabadiliko makubwa yaliyopatikana katika siku za hivi karibuni kutokana na mahakama kuendelea kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa utoaji wa elimu ya utoaji haki na sheria kwa umma tofauti na ilivyokuwa zamani.

Jaji Aboud amesema Mabadiliko hayo amesema yamefikiwa baada ya kuwepo viashiria kadhaa
ikiwemo kupungua kwa malalamiko, mwamko wa umma kuongezeka ambapo
idadi kubwa ya wananchi sasa wanaenda  mahakamani kutafuta haki zao badala ya kujichukulia sheria mkononi.

JAJI Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Tanga ametoa kauli hiyo wakati akijibu swali la mwandishi wa blog hii  mara baada ya kutoa taarifa kwa vyombo vya Habari  kuhusu ratiba ya Maadhimisho ya wiki ya Sheria ambapo kimkoani hafla ya uzinduzi itafanyika asubuhi ya kesho- 28/1/2017 katika viwanja vya Mahakama kuu iliyopo jijini Tanga.

"Tukio hili linaashiria kuanza rasmi kwa shughuli za mahakama kwenye mwaka husika na katika kuifanikisha tayari mahakama imeanza kuratibu utoaji wa elimu ya haki na sheria kwa umma ambapo mada mbalimbali huwasilishwa kupitia Radio na madawati maalum ya ushauri yaliyopo kwenye viwanja vya mahakama zote zilizopo kanda hii ili kuwapa fursa wananchi kushauriwa, kufahamishwa haki zao na kuelekezwa namna ya kuzidai kwa wakati ili kuharakisha maendeleo ,"alisema.

Aliongeza, "Mahakama baada ya kutekeleza maboresho katika utendaji wake wa kila siku hupokea mrejesho wa mara kwa mara kutoka kwa jamii na tumeona yapo mabadiliko makubwa katika miaka ya hivi karibuni ambapo wananchi wanaonesha mwamko wa kutafuta haki zao mahakamani tofauti na zamani, ".

Jiji Mfawidhi huyo alisema kuongezeka mahakamani kwa idadi ya kesi za jinai, mirathi na madai ni miongoni mwa viashiria vinavyothibitisha mafanikio hayo kutokana na mwendelezo wa mpango wa utoaji wa elimu ya haki na sheria kwa umma unaoratibiwa na Mahakama kwa kushirikiana na wadau wake kila mwaka.

"Jaji mfawidhi amesema Kesi nyingi hivi sasa hazichukui muda mrefu wa kusikilizwa kwasababu tumejiwekea lengo maalum kwamba ndani ya siku 90 uamuzi uwe umetolewa, kutokana na maboresho hayo imefikia wakati sasa baadhi ya mawakili wanalalamika kuhusu kasi hii tunayoenda nayo lakini hatuna namna ni lazima haki ipatikane kwa wakati ili kuwezesha ukuaji wa uchumi wa jamii na taifa kwa jumla, " alisema Jaji Aboud.

Aidha,  amesema mkuu wa mkoa wa Tanga, Martine Shigella anatarajiwa kutoa hotuba ya ufunguzi na hivyo kutoa wito kwa wakazi kujitokeza kwa wingi katika maadhimisho hayo.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni