SILAHA ya kivita aina ya SMG na risasi 30 mali ya Hifadhi ya Taifa
ya Saadani vimekutwa vimefichwa kwenye kichaka jirani na Mto Kitame katika Kata
ya Makurunge wilayani Bagamoyo, Mkoa wa Pwani.
Silaha hiyo inadaiwa iliibiwa kwenye Geti la Gama saa tisa
usiku Desemba 24, mwaka jana wakati askari wa hifadhi hiyo, Jackson Shirima
(23) akiwa kazini.
Kamanda wa Polisi mkoani humo, Bonaventura Mushongi amesema
tukio hilo lilitokea muda mfupi baada ya askari huyo kutoka zamu ya lindo la
geti hilo na kujipumzisha kwenye moja ya mahema akiwa na silaha hiyo.
“Huyu
askari alikuwa zamu na kama ilivyo ada huwa wanapokezana zamu ya ulinzi hivyo
alitoka na silaha yake akaenda kujipumzisha kwenye hema maana hifadhini hutumia
mahema na alipitiwa na usingizi na ndipo ilipoibiwa na mtuhumiwa aliyewahi kuwa
mtumishi wa hifadhi hiyo,”
alisema.
Mushongi alibainisha kuwa baada ya wizi huo, askari kwa
kushirikiana na Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (Tanapa) walianza msako na kupitia
taarifa ya msamaria mwema walimkamata mtuhumiwa huyo, mkazi wa Tegeta Kibaoni
ambaye alikwenda kuonyesha alipokuwa ameificha kichakani ikiwa na risasi
30.
Mkuu wa hifadhi hiyo, Dk James Wakibara alisema wameshtushwa
na tukio hilo kwani halijawahi kutokea na kwamba, zaidi ni baada ya kukuta
mtuhumiwa huyo aliwahi kuwa mtumishi wao na aliacha kazi miezi kadhaa iliyopita
yeye mwenyewe.
Dk Wakibara alilishukuru Jeshi la Polisi kwa ushirikiano
lilioutoa toka siku ilipoibiwa silaha hiyo hadi ilipopatikana.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni