WAKALA wa barabara (TANROADS)mkoani Pwani ,umeanza
zoezi la bomoabomoa kuanzia eneo la Kiluvya Darajani hadi
Mailmoja-Kibaha,ambapo limefanikiwa kwa asilimia zaidi ya 70 hadi sasa.
Zoezi hilo ni la siku tatu kuanzia Jan 23 hadi 25
lengo likiwa kupisha hifadhi ya barabara urefu wa mita 60.
Aidha bomoabomoa hiyo haitogusa eneo la soko la
nafaka na baadhi ya mabucha ya nyama kutokana na soko jipya la nafaka
kutokamilika hadi februari 15 hivyo kuendelea kusaidia wananchi kupata mahitaji
yao muhimu.
Akizungumzia zoezi hilo linavyoendelea,meneja wa
TANROADS Pwani,injinia Yudas Msangi,alisema wanalenga kubomoa nyumba za
biashara 165,vibanda 84,nyumba za kuishi watu 10 na soko kuu la Mailmoja.
“Hadi kufikia leo mpango wetu unaenda vizuri sana
,tumeshafikia asilimia zaidi ya 70, na hii imetokana na kutokuwa na mtu wa
kulalamika wala kuilaumu TANROADS”
“Tuliwapa taarifa mapema na wengi wametii kwa
kuvunja wao wenyewe na kutoa vitu vyote vya thamani licha ya wachache ambao
walishindwa kubomoa wao wenyewe,” alisema injinia Msangi.
Injinia Msangi,alieleza ,Maili Moja ndiyo
imehitimisha zoezi la ubomoaji kwa watu waliojenga kwenye hifadhi ya barabara
katika mkoa huo ambapo mwaka 2015 walibomoa maeneo mengine ya wilaya zote za
mkoa.
Mkaguzi wa barabara, Injinia Livingstone Urio
alisema huo ni mwendelezo wa usafishaji wa maeneo ya hifadhi ya barabara na
kuweka usalama kwa wananchi kwani ni hatari kujenga ama kufanya biashara karibu
na barabara.
Nae mkuu wa mkoa wa Pwani,mhandisi Evarist
Ndikilo,alisema nia ya serikali sio kuona wananchi wanatangatanga bali ni
kuwajengea mazingira na miundombinu bora ili waendeshe shughuli zao .
Alieleza kwamba ,hataki kuona mtu anajipenyeza
kwenye maeneo ambayo tayari yamevunjwa.
Mhandisi Ndikilo alisema, Mji wa Kibaha umeshakua na
kupanuka ukielekea kuwa manispaa hivyo hainabudi kufungua mianya ya kibiashara
na njia kubwa za barabara ikiwemo Kisarawe na Bagamoyo ili kuinua soko
lake.
Diwani wa kata ya Mailmoja,Ramadhani
Lutambi,alimpongeza mhandisi Ndikilo kwa kushirikiana na Tanroads kutoa elimu
hivyo kuepusha malalamiko ambayo huwa yakijitokeza wakati wa bomoabomoa nchini.
Alisema haijawahi kutokea zoezi kama hilo likaenda
kimya kimya na watu kuondoa vifaa vyao bila shuruti kama Mailmoja.
Hata hivyo,Lutambi alisema kuna changamoto
imejitokeza kwa baadhi ya wafanyabiashara ambao wamekosa maeneo soko jipya la
Mnarani,ambalo limetengwa na halmashauri.
Alibainisha kuwa soko jipya ni dogo, halitoshelezi
mahitaji,frem za biashara zilizobomolewa ni 165,zilizopo 110 sokoni hapo huku
wajasiriamali wakiwa ni 400 na soko hilo likiwa na nafasi aya watu 200.
Lutambi alisema, lazima wengine watakosa nafasi na
ndio maana malalamiko ni makubwa hivyo anawasiliana na halmashauri,wilaya na
mkoa ili kuona namna ya kusaidia watakaokosa na kutenda haki bila upendeleo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni