Jumanne, 3 Januari 2017

WANAWAKE ZANZIBAR WAITAKA SERIKALI KUPUNGUZA ADA YA USAJIRI ARDHI.


SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar imetakiwa kupunguza gharama za usajili wa ardhi kwa wanawake ili waweze kufikia na kumiliki ardhi na hivyo kuleta usawa wa kijinsia.

Amezungumza hayo Mratibu wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (Tamwa) Zanzibar, Dk Mzuri Issa alisema wanawake wengi wamehamasika kujitokeza kupata hatimiliki lakini tatizo la urasimu na gharama kubwa za ada ni moja ya kikwazo kinachowakabili na kuwarudisha nyuma wanawake.

Kwa mfano alisema maombi 101 ya usajili wa ardhi yamefikishwa katika mamlaka mbalimbali ikiwemo kwa masheha katika hatua za awali pamoja na mamlaka ya ardhi katika hatua za mwisho lakini malalamiko makubwa yaliyojitokeza ni gharama kubwa.

“Tunashauri ni vizuri kwa serikali kupitia tena sera ya ardhi ili kuona mikataba ya kimataifa inavyolenga kutoa usawa wa kijinsia na kupunguza umasikini kwa jamii ya mwanamke,” alisema.

Alisema gharama za usajili zinazofikia sh 200,000 ni kubwa kuanzia kwa sheha hadi wilayani na katika Kamisheni ya Ardhi na watu wanaowasilisha maombi hayo kukwama katika hatua hizo.

Alisema pamoja na juhudi kubwa za kuimarisha ufikiwaji na umiliki wa ardhi kwa wananchi, rasilimali ya msingi ya maendeleo ni kiasi cha asilimia 20 tu cha wanawake ndiyo watakaofikiwa na huduma za umiliki wa ardhi.

Tamwa visiwani Zanzibar kwa kushirikiana na mashirika ya kimataifa kipo katika juhudi za kutoa elimu kwa wanawake kuona wanafaidika na fursa za kumiliki ardhi kwa maendeleo ya taifa na kiuchumi kwa ujumla.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni