Jumatano, 18 Januari 2017

KAIMU KATIBU MTENDAJI WA TUME YA MIPANGO, FLORENCE MWANRI AFANYA ZIARA KUANGALIA SHUGHULI ZA UZALISHAJI WA SARUJI KATIKA KIWANDA CHA TANGA CEMENT.





Meneja wa Kiwanda cha Tanga Cement, Mhandisi Ben Lema mwenye Miwani, akimwonesha Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango, Bibi Florence Mwanri  Wengine ni Maofisa wa Ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo walioambatana na Kaimu Katibu Mtendaji katika ziara hiyo.

Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango, Bibi Florence Mwanri akikagua mifumo ya kisasa inayotumika kuendesha shughuli mbalimbali katika kiwanda cha Tanga Cement.
 Baadhi ya mitambo inayoendelea kufanya kazi katika kiwanda cha Tanga Cement.

 
 
TANGA

Timu ya ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo kutoka Tume  ya Mipango ikiongozwa na Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume hiyo, Bibi Florence Mwanri imefanya ziara katika Kiwanda cha Tanga Cement kilichopo Mkoani hapa kwa lengo la kukagua shughuli mbalimbali zinazofanywa na kiwanda hicho.

Katika ziara hiyo, Bibi Mwanri amepata fursa ya kukagua maeneo mbalimbali ya kiwanda hicho ikiwa ni pamoja na eneo linalotumika kuchimba malighafi za kutengenezea saruji, teknolojia ya kisasa inayotumika kuendesha mashine kiwandani hapo pamoja na kuangalia hatua mbalimbali zinazotumika katika uzalishaji wa saruji.

Akiwa katika eneo linalochimbwa mawe ya kutengenezea saruji, Mwanri ameeleza kuwa kiwanda hicho kina wajibu wa kuhakikisha sheria  na taratibu za utunzaji wa mazingira zinazingatiwa muda wote ili kuhakikisha mazingira yanabaki salama licha ya shughuli za uchimbaji kuendelea kufanyika.

Mwanri amepongeza uongozi wa kiwanda hicho kwa kuendelea kutekeleza majukumu yake katika kuunga mkono dhamira ya Serikali ya kuwa nchi ya Viwanda na kuharakisha malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo inayosisitiza kufikia uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.

Naye Meneja wa Kiwanda hicho, Mhandisi Ben Lema amesema kiwanda hicho kimeendelea  kutoa ajira kwa watanzania katika kada mbalimbali ambapo kwa sasa kua ajira zaidi ya 600 ambapo ajira 300 ni za moja kwa moja huku ajira 300 zingine ambazo sio za moja kwa moja zinajumuisha wauzaji, wasambazaji, wasafirishaji na wengine walioko katika mnyororo huo.

Ameongeza kuwa bidhaa za kiwanda hicho bado zinafanya vizuri sokoni licha ya ushindani uliopo kufuatia kuanzishwa kwa viwanda vingi vinavyozalisha saruji kwa kuwa mahitaji ya saruji bado ni mwakubwa sokoni.



Lema amesema viwanda vya saruji vinapata faraja kubwa kwa kuwa miradi mbalimbali ya ujenzi inayotekelezwa na Serikali na hata inayotekelezwa na sekta binafsi inatumia saruji inayotengenezwa na viwanda vya ndani ya nchi.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni