MASHITAKA 10
yaliyofunguliwa na walei 32 wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Dar es Salaam
yakiwemo ya ufisadi wa mali za kanisa, yamesababisha Askofu Mkuu wa Kanisa la
Anglikana Tanzania Dk Jacob Chimeledya kumvua uaskofu Mkuu wa Dayosisi ya Dar
es Salaam Dk Valentine Mokiwa.
Hata hivyo Dk Mokiwa amegomea uamuzi huo kwa maelezokuwa mwajiri wake ni Sinodi ya Dar es Saalam ambayo ndiyo yenye uamuzi wa kumfuta kazi na sio askofu mkuu au askofu mwingine yeyote wa kanisa la Anglikana Tanzania.
Uamuzi wa kumvua uskofu ulichukuliwa
juzi na Askofu Chimeledya baada ya Askofu Mokiwa kugoma kujiuzulu kama
ilivyoshauriwa na nyumba ya maaskofu ambayo ilimkuta na hatia ya kufuja mali za
kanisa hilo na kukiuka maadili ya kichungaji ambayo yalibainishwa kwenye ripoti
ya uchunguzi iliyoundwa na kiongozi mkuu wa kanisa hilo nchini.
Habari zilizopatikana kutoka ndani
ya kanisa hilo zilieleza kuwa katika kikao kilichofanyika juzi kanisani Ilala,
askofu Chimeledya na ujumbe wake walihudhuria kikao cha halmashauri ya kudumu
ya dayosisi ya Dar es Salaam akatangaza uamuzi wa kumvua uaskofu Dk Mokiwa
chini ya ulinzi wa polisi.
Licha ya uamuzi wa kumvua uaskofu,
Dk Chimeledya pia aliagiza waraka unaoagiza askofu huyo kuondolewa madarakani,
usambazwe kwenye makanisa yote yaliyoko chini ya dayosisi ya Dar es Salaam na
usomwe jana kwenye ibada mbele ya waumini.
“Ni kweli kikao hicho kilifanyika
jana, Dk Chimeledya alikuja na katibu mkuu na msajili wa kanisa kwenye kikao,
lakini tulishangaa kwamba walikuja na askari polisi kinyume na utaratibu wa
kanisa, alisoma maamuzi hayo aliyodai yametolewa na nyumba ya maaskofu,”alisema msemaji wa Dayosisi ya Dar es Salaam Yohana Sanga.
Dk Mokiwa agoma kung’oka
Katibu Mkuu wa Dayosisi ya Dar es
Salaam Padri Jonathan Senyagwa jana alisema habari hizo sio za kweli na barua
ambazo zimesomwa katika baadhi ya makanisa jijini Dar es Salaam zilisomwa kwa
makosa.
“Mwenye mamlaka ya kumfukuza kazi ni
yule aliyemwajiri, na mwajiri wa Dk Mokiwa ni Sinodi ya Dar es Salaam...tutatoa
tamko hivi karibuni kuthibitisha kwamba askofu wa jimbo bado hajafukuzwa,” alisema Padri Senyagwa.
Alisema waraka ambao umesambazwa na
askofu mkuu wa Tanzania haujapitia kwenye halmashauri ya kudumu ya dayosisi ili
kupata baraka zake na wala hauna baraka kutoka kwa sinodi ya dayosisi jambo
ambalo linaufanya waraka huo ukose sifa za kutekelezeka.
“Ninachokwambia ni kwamba askofu wa
dayosisi ya Dar es Salaam bado ni Mokiwa, hatuzitambui barua zilizosomwa katika
baadhi ya makanisa,” alisisitiza katibu mkuu huyo wa
Dayosisi.
Mgomo huo pia ulithibitishwa na
Sanga, ambaye alifafanua kuwa juzi kulifanyika kikao kati ya viongozi wakuu wa
kanisa na halmashauri ya kudumu ya dayosisi ya Dar es Salaam na kuelezwa na
askofu mkuu wa Tanzania Dk Chimeledya hatua ya kumvua uaskofu Dk Mokiwa jambo
ambalo halmashauri iligoma.
“Tulifanyia kikao chetu pale kanisa
la Ilala, viongozi wetu wakuu walikuja na polisi wakatusomea huo waraka na
kutangaza maamuzi hayo mbele ya halmashauri, lakini maamuzi hayo yaligomewa na
wajumbe wa halmashauri ya Dayosisi ya Dar es Salaam,” alisema Sanga.
Alisema halmashauri iligoma kubariki
uamuzi huo kwa sababu kanisa la Anglikana Tanzania lina kanuni na taratibu
zake.
Alifafanua kuwa waraka wa kumwondoa
madarakani Dk Mokiwa lazima upate baraka za halmashauri ya kudumu ya dayosisi
na sinodi ya dayosisi.
“Ule waraka tuliupitia na kubaini
kuwa hauna baraza za nyumba ya maakofu, wala hauna baraka za halmashauri ya
kudumu na Sinodi ya dayosisi ndio maana tuliwakatalia,” alisema Sanga na kuongeza kuwa maamuzi ya kumvua uaskofu Dk
Mokiwa yamefanywa na askofu mkuu wa Tanzania, katibu mkuu na msajili wa kanisa
na sio vikao vya kanisa.
“Ninachosisitiza hapa ni kwamba
askofu wa dayosisi ya Dar es Salaam bado ni Dk Mokiwa, huo waraka uliotangazwa
ni ushawishi wa watu wachache wanaotaka kumchafua kiongozi wetu wa Dayosisi,” alisema.
Aombwa ajiuzulu uaskofu
Awali tume hiyo iliyoundwa
kuchunguza tuhuma dhidi yake, baada ya kubaini makosa mengi yaliyofanywa na
askofu huyo ilimshauri ajiuzulu wadhifa wake na awe tayari kufanya huduma
nyingine ya kumtumikia Mungu.
“Hatua tunayoichukua ni kwa nia
njema kabisa ya kulinusu kanisa letu ambalo limekuwa naheshima kubwa hapa
nchini na duniani kote,” unasema
waraka uliosaniwa na Dk Chimeledya.
Tume hiyo ilichukua uamuzi huo
katika kutatua mgogoro uliopo ndani ya dayosisi ya Dar es Salaam:
“Nia yetu ni njema kabisa na hatuna
chuki, uhasama wala upendeleo katika jambo hili, ifahamike kuwa vyombo vyote
ndani ya kanisa ikiwemo nyumba ya maaskofu vinalifahamu jambo hili vyema, hivyo
tulitarajia tutaungwa mkono ili kuisaidia dayosisi yetu ya Dar es Salaam kwenda
mbele.”
Pia waraka huo unaeleza kuwa hiyo
sio mara ya kwanza kanisa hilo kufanya maamuzi ya namna hiyo na kutoa mfano
kuwa hata enzi za askofu Mokiwa akiwa askofu mkuu wa Tanzania alichukua hatua
za kulinusuru kanisa lisipotee katika migogoro mbalimbali ikiwemo mgogoro wa
dayosisi ya Tanga ambako alimtaka askofu wa dayosisi hiyo ajiuzulu kwa hiyari
na alikubali.
Baada ya kutenguliwa uaskofu wa
Mokiwa, Dayosisi ya Dar es Salaam itakuwa chini ya uangalizi wa uongozi wa
askofu mkuu mpaka taratibu nyingine za kikanuni zitakapokamilika.
“Nina wasii Wakristo wote kwa nieaba
ya Bwana Yesu Kristo tuendelee kuwa watulivu katika kuijenga dayosisi yetu na
kanisa la Mungu kwa ujumla.”
Mashitaka 10 ya Mokiwa
Askofu Mokiwa Machi 2015
alifunguliwa mashitaka 10 ambayo ni kuizuia dayosisi ya Dar es Salaam kupeleka
michango pasipo maelekezo ya sinodi ya Dayosisi ya Dar es Salaam, kuhamasisha
dayosisi kujitoa katika udhamini wa kanisa Anglikana Tanzania (KAT) kwa lengo
la kuifarakanisha dayosisi na jimbo kinyume na katiba ya dayosisi.
Mashitaka mengine ni kufuja mali za
kanisa na kuingia mikataba kiholela yenye viashiria vya rushwa katika eneo la
kanisa la mtoni Buza na miradi mingine, kushindwa kutatua migogoro inayohusu
uwekezaji na maadili baina ya dayosisi na mitaa ya Magomeni ambao kuna mgogoro
na Benki ya DCB, kanisa la Kurasini na mengine.
Askofu huyo pia anadaiwa kushindwa
kutatua migogoro baina ya mapadiri na waumini na kutunza mali za kanisa katika
mtaa wa Watakatifu wote Temeke na kutelekeza nyumba ya askofu iliyopo Oysterbay
ambako imegeuzwa kuwa yadi ya kuuza magari.
Pia alilalamikiwa kushitakiwa
mahakamani na Marehemu Christopher Mtikila na watu wengine watatu kwa kosa la
kuwatishia silaha ya moto na kuwapapasa maungoni mwao bila ridhaa yao kinyume
na maadili ya kikanisa.
Askofu Mokiwa pia analalamikiwa
kuanzisha taasisi ya MEA Foundation iliyomwezesha kupokea fedha nyingi za
wafadhili kwa ajili ya maendeleo ya dayosisi, lakini fedha zimefujwa na hesabu
za chombo hazikuwahi kukaguliwa.
Tuhuma zingine ni kurejea kwa
mchakato wa mapitio ya katiba mpya na kuvuruga mchakato wa awali wa maandalizi
ya katiba mpya ya dayosisi kwa kutumia fedha za dayosisi na kutekelezwa askofu
msaidizi dayososi ya Katanga Kalemi .
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni