WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amesema nchi haijakumbwa na baa la njaa na
amewataka Watanzania kutosikiliza kampeni za upotoshwaji zinazofanywa na
baadhi ya wafanyabiasha kuhusu hali ya chakula kwani si za kweli bali
ni za uzushi zenye lengo la kupandisha bei za vyakula.
Amesema
Serikali ndio yenye jukumu la kutoa taarifa za kuwepo kwa njaa ama
kutokuwepo na kwamba taarifa zinazosambazwa za kuwepo kwa baa la njaa
nchini hazina ukweli wowote na Serikali inawahakikishia wananchi kuwepo
kwa usalama wa chakula.
Waziri
Mkuu ametoa kauli hiyo leo (Jumatatu, Januari 16, 2017) wakati
akizungumza na waandishi wa habari mkoani hapa Dodoma baada ya kuzindua
safari za ndege za Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) kutoka Dar es Salaam
kwenda Dodoma, ambapo amesisitiza kwamba hali ya upatikanaji chakula
nchini ni tofauti na inavyoelezwa na baadhi ya vyombo vya habari.
Waziri
Mkuu ametoa kauli hiyo baada ya kutolewa kwa taarifa katika vyombo
mbalimbali vya habari kuhusu kuwepo kwa baa la njaa nchini jambo ambalo
si la kweli. Amewataka wananchi kuwa watulivu na jambo hilo likitokea
Serikali itatoa taarifa.
“Mwaka
jana nchi ilikuwa na akiba ya chakula cha zaidi ya tani milioni tatu
hali iliyopelekea baadhi ya Wabunge na wafanyabiashara kuomba kibali cha
kuuza nafaka nje ya nchi, ambapo Serikali ilitoa kibali hicho baada ya
kujiridhisha kuwepo kwa akiba ya kutosha ya chakula,” amesema.
Amesema
baada ya kutolewa kwa kibali hicho tani milioni 1.5 ziliuzwa nje ya
nchi na Kiasi cha tani milioni 1.5 zilizobaki zilihifadhiwa kama akiba
ambapo tayari wameruhusu ziuzwe hapa nchini ili kupunguza kupanda kwa
bei za vyakula nchini.
“Naomba
wananchi msiwe na wasiwasi juu ya hali ya chakula nchini. Msisikilize
kelele zinazopigwa na watu mbalimbali pamoja kwenye baadhi ya vyombo vya
habari yakiwemo magazeti kwani taarifa hizo si za kweli. Chakula kipo
cha kutosha licha ya mvua kusuasua katika baadhi ya maeneo nchini,” amesema.
Hata
hivyo Waziri Mkuu amesema kuwa kwa sasa mvua zimeanza kunyesha katika
maeneo mbalimbali nchini, hivyo amewaomba wananchi kuzitumia kwa kulima
mazao ya muda mfupi yanayostahimili ukame.
Waziri
Mkuu amesema kwamba endapo kutatokea uhaba wa chakula nchini, Serikali
itatoa utaratibu wa namna ya upatikanaji wa chakula kwa wananchi wake.
Kuhusu kupanda wa bei ya vyakula katika baadhi ya masoko amesema inatokana na kuwepo kwa uhaba wa chakula katika nchi jirani.
Aidha,
Waziri Mkuu amesema kwamba Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, itatoa
taarifa kuhusiana na hali halisi ya chakula nchini kwa sasa na pia
itatoa taarifa kuhusu hali ya mvua ili Watanzania waweze kupata ukweli
wa hali ilivyo.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni