Alhamisi, 5 Januari 2017

SHULE YA NAIBU WAZIRI WA JK,MAHIZA INAMADARASA MATATU PEKEE ,HUKU IKIWA NA MIKONDO SABA


SHULE  ya msingi iliyopewa jina la aliyekuwa naibu waziri  wa elimu wakati wa utawala wa Rais mstaafu Jakaya  Kikwete ,Mwantumu Mahiza mpaka  sasa inamadarasa matatu pekee hali inayosababisha wanafunzi wengine kusoma chini ya miti.

Shule iliyoko wilayani Mkinga mkoani Tanga inawanafunzi kuanzia darasa la kwanza hadi la saba  ambao hulazimika kusomea katika chumba kimoja kwa kupokezana na huku wengine wakipata elimu  chini ya miti. 

Hayo yamesababisha na Afisa Elimu msingi wilayani humo Zakayo Mrindoko wakati akiongea na Mtanzania kueleza changamoto za miundombinu ya kielimu inayoikabili   wilaya hiyo kwa sasa 

Alisema kuwa  shule hiyo ni miongoni mwa shule 11 zilizoanzishwa wakati wa mradi wa Mpango wa maendeleo ya Elimu ya msingi MMEM ambazo mpaka sasa zimeshindwa kuendelezwa kutoka na Halmashauri  kukosa fedha za kuendeleza majengo ya shule hizo pamoja na ofisi za walimu. 

Afisa Elimu huyo alisema kuwa uhaba huo wa vyumba vya madarasa wakati mwingine hulazimu wanafunzi wa madarasa mawili kusoma katika chumba kimoja jambo ambalo linaleta usumbufu  katika  utoaji wa elimu. 

Alisema kuwa ili miundombinu ya shule nyingi wilayani humo iweze kuwa vizuri na wanafunzi waweze kupata elimu katika mazingira bora kuna hitajika kiasi cha shilingi Bilioni mbili ambazo zitatumika kujenga madarasa 86..

"Kwa upande wa madawati hakuna shida ila tatizo kubwa lipo kwenye uhaba  wa madaraka, ofisi za walimu pamoja na watumishi kwa maana ya walimu ikama yao ni ndogo kwani tunaupungufu wa walimu 288 wa kada zote"alibainisha.

Hata hivyo Kaimu Mkurugenzi  wa Halmashauri  hiyo Michael Ndunguru alisema kuwa licha ya changamoto  za miundombinu zilizoko kwenye upande wa elimu wamefanikiwa kuvuka lengo la uandikishaji  wa wanafunzi wa darasa la kwanza kwa zaidi  ya 150%.

Alisema kuwa mwitikio huo umekuwa mkubwa kutoka na sera ya elimu bure inayotekelezwa kwa sasa nchini hivyo hata wazazi ambao kipato chao ni kidogo wameweza kuleta watoto wao. 

"Kwa hili la miundombinu  tumejipanga kuwaita wadau wa maendeleo  pamoja na wakazi wa wilaya hii waishio nje ya wilaya waweze kuchangia maendeleo  ya kielimu ili watoto wao waweze kupata elimu katika mazingira  bora badala  ya kusubiri serikali pekee"alisema Kaimu Mkurugenzi  huyo.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni