Alhamisi, 12 Januari 2017

SERIKALI HAINA CHAKULA CHA MSAADA ASEMA RAIS MAGUFULI..



RAIS John Magufuli amesema inawezekana asiwe mwanasiasa mzuri, lakini siku moja atakumbukwa kwa mambo ambayo anayafanya, kwa sababu dhamira yake ni nzuri katika kusimamia ubadhirifu wa fedha za umma na kusimamia miradi ya maendeleo ili watanzania wote wanufaike.

Pia amesisitiza kuwa serikali haitatoa chakula cha msaada kwa wananchi. Aidha, katika kusimamia kauli zake mkoani Simiyu, Rais Magufuli ameagiza hospitali ya rufaa ya mkoa wa Simiyu ambayo aliweka jiwe la msingi, ujenzi wake jana kujengwa kwa Sh bilioni 10 na kukataa kiwango kilichokuwa kimekadiriwa cha Sh bilioni 46.

Rais Magufuli alitoa kauli hiyo jana katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya shule ya msingi Somanda wilayani Bariadi, kabla ya kwenda kuzindua ujenzi wa barabara.

Awali Rais alikuwa na mikutano mingine katika vijiji vya Nyashimo, Masanzakona, Lamadi na Nyamikoma wilayani Busega mkoani Simiyu katika siku ya kwanza ya ziara yake mkoani humo.

“Nimeweka jiwe la msingi katika ujenzi wa hospitali, ujenzi wake wamesema ni Shilingi bilioni 46, nimesema kitu hicho hakiwezekani, tena wamekosea sana kuniita mimi kuja kuweka jiwe la msingi,” alisema Rais Magufuli.

Ujenzi wa hospitali hiyo ambayo inajengwa na Wakala wa Majengo ya Serikali (TBA), Rais Magufuli alikataa gharama alizoelezwa, kwa maelezo kuwa ni kubwa.

“Haiwezekani pale Chuo Kikuu Dar es Salaam majengo yote yale yalijengwa kwa Sh bilioni 10, hapa jengo moja Sh bilioni 46, haiwezekani hata kidogo, nitaleta shilingi bilioni 10 kutoka ndani ya Serikali na hospitali hiyo ikamilike,” alisema.

Rais Magufuli alisema amekaa katika sekta ya ujenzi kwa zaidi ya miaka kumi, ambapo alisema Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ina majengo 20 yenye ghorofa nne ambazo zilijengwa kwa Sh bilioni 10.

“Mkitaka mkalete majengo yale ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mbandike hapo, mtajua, nyie jengo hilo moja tena la ajabu ajabu, mnasema bilioni zote hizo, haiwezekani na siku ya kuzindua nitakuja mimi,” alisema.

Rais Magufuli alisema fedha za ujenzi wa barabara hiyo zote, zimetolewa na Serikali ambapo alimuagiza Waziri Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa kilometa 48.9 zilizobaki katika barabara hiyo ndani ya wiki moja, ziwe zimetangazwa kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami.

Alisema kwa kujengwa barabara hiyo, wananchi wa mkoa huo wataweza kufanya biashara kwa urahisi, ambapo amewaomba wananchi kuitumia vizuri barabara hiyo na kuilinda.

“Imekuwa ni kawaida barabara ikijengwa inakuwa chanzo cha ajali, watu wanaendesha kwa fujo, badala ya barabara kuwatunza inakuwa ndio chanzo cha mauaji, natoa mwito tuzingatie sheria za barabarani nisije kusikia baada ya siku chache imeua,” alisema.

Rais Magufuli aliwataka wananchi ambao wako ndani ya mita 2.5 kila upande, eneo ambalo barabara hiyo itapita, waanze kuondoka, wasiwe chanzo cha ucheleweshaji wa mradi huo.

Rais alisema pia kuwa kuna baadhi ya wafanyabiashara na wanasiasa, wanadai kuwa kuna njaa nchini, ambapo alisema kuwa kama kuna njaa, ni yeye atatoa tamko hilo.

“Wapo wafanyabiashara wachache waliokuwa wamezoea panatokea ukame kidogo, wanatumia vyombo vya habari vichache na baadhi ya wanasiasa kuzungumza Tanzania kuna njaa, lengo lao wasamehewe kodi,” alisema.
Alisema wafanyabiashara hao, wameleta mahindi yaliyo katika ubora usiofaa kwa lengo la kuuza bila kulipa kodi ili wapate faida.

“Yupo mfanyabiashara mmoja ameleta tani 25,000 za mahindi, anataka tumsamehe kodi, tumeshamkata kodi na huo ndio mchezo wao, wanawaambia andikeni kuna njaa, anayejua kuna njaa ni Rais,” alisema Rais Magufuli.
Alisema wabunge mwaka jana wakiwa katika vikao vya Bunge, walisema chakula ni kingi na kushauri kiuzwe nchini Uganda, lakini sasa hivi wanadai kuwa chakula hakitoshi.

Hivi karibuni Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo na Mbunge wa Kigoma Mjini, Kabwe Zitto, aliitaka Serikali itangaze rasmi baa la njaa kwa mujibu wa sheria.

Zitto alitoa kauli hiyo katika mkutano wa hadhara wa kumnadi mgombea udiwani wa Kata ya Nkome mkoani Geita kupitia ACT-Wazalendo, ambapo alisema bei ya chakula inazidi kupanda kutokana na uhaba wa chakula.

Rais Magufuli alisisitiza kuwa serikali haitatoa chakula cha msaada kwa wananchi hata kidogo, na kueleza kuwa jukumu la serikali siyo kugawa chakula cha bure kwa wananchi.

Alisema kuwa serikali haiwezi kutoa chakula cha msaada kwa watanzania zaidi ya milioni 50 nchi nzima, huku akiwataka wananchi kutowasikiliza wanasiasa ambao wanafanya siasa za kizamani.

“Jukumu la Serikali sio kuleta chakula kwa sababu serikali haina shamba la kulima, ni lazima niwaambie ukweli na ukweli utabaki kuwa ukweli, na wanasema asiyefanya kazi na asile…. maana yake na asipokula si afe, niwaombe mfanye kazi,” alisema Rais Magufuli.

Alibainisha kuwa kazi kubwa ya serikali ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za fya, barabara, maji, umeme pamoja na elimu, na siyo kutoa chakula cha bure.

Rais alisema kuna maeneo hapa nchini, ambayo mvua zimenyesha na hazikutosha, hivyo wananchi wajipange kulima mazao ambayo hayatahitaji maji mengi na pia kuchukua muda mrefu kabla ya kuvunwa na sio kwamba kuna njaa.

“Ninafahamu wapo wanasiasa wachache ambao wanafikiri mzee bure hajatoka kichwani kwao, kila kitu kikitokea serikali ifanye, serikali ninayoiongoza mimi haitatoa kitu, mlinichagua niwaeleze ukweli na mimi nawaeleza ukweli,” alisema Magufuli.

Aliongeza kuwa bado hajachoka kuendelea kutumbua watumishi wanaowanyonya wananchi wanyonge, ambao wanakula rushwa bila huruma pamoja na mafisadi.

Alisema ataendelea na utaratibu huo. Rais Magufuli leo anaendelea na ziara yake mkoani humo kwa siku ya pili, ambapo atatembelea kiwanda cha chaki wilayani Maswa, ikiwemo kuweka jiwe la msingi barabara ya Maswa Mwigumbi, Shinyanga.

Awali katika mikutano yake mkoani humo, Rais Magufuli akiwa Busisi mkoani Mwanza, alisisitiza kutotoa msaada wa chakula kwa kaya zinazokabiliwa na tatizo la njaa nchini.

Aliwataka wananchi kuzitumia vyema mvua zinazoendelea kunyesha kwa kulima mazao yanayostahimili ukame, badala ya kutegemea msaada wa chakula kutoka serikalini.

Wakati huo huo, viongozi wa Wilaya ya Kongwa walitakiwa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Jordan Rugimbana kulima mazao yanayostahili ukame ya mtama na muhogo ili kuondokana na njaa inayotaka kuanza kunyemelea wilaya hiyo.

Rugimbana alitoa kauli hiyo mwishoni mwa wiki wakati wa ziara wilayani humo, ambapo alizungumza na kada mbalimbali za viongozi ikiwamo kamati ya ulinzi na usalama, watendaji wa halmashauri, viongozi wa CCM na walimu.

Mkuu wa Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga, Fadhili Nkurlu akizungumza na waandishi wa habari naye aliwataka wananchi wa wilaya yake kutunza chakula pamoja na kukitumia vizuri kiasi kidogo kilichopo na kuwataka wananchi kupanda mazao yanayostahimil ukame.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni