Ijumaa, 27 Januari 2017

SHEREHE YA SIKU YA SHERIA KUANZA RASMI KESHO MKOANI TANGA.

JAJI Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Tanga, Mhe. Imani Aboud amesema yapo mabadiliko makubwa yaliyopatikana katika siku za hivi karibuni kutokana na mahakama kuendelea kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa utoaji wa elimu ya utoaji haki na sheria kwa umma tofauti na ilivyokuwa zamani.

Jaji Aboud amesema Mabadiliko hayo amesema yamefikiwa baada ya kuwepo viashiria kadhaa
ikiwemo kupungua kwa malalamiko, mwamko wa umma kuongezeka ambapo
idadi kubwa ya wananchi sasa wanaenda  mahakamani kutafuta haki zao badala ya kujichukulia sheria mkononi.

JAJI Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Tanga ametoa kauli hiyo wakati akijibu swali la mwandishi wa blog hii  mara baada ya kutoa taarifa kwa vyombo vya Habari  kuhusu ratiba ya Maadhimisho ya wiki ya Sheria ambapo kimkoani hafla ya uzinduzi itafanyika asubuhi ya kesho- 28/1/2017 katika viwanja vya Mahakama kuu iliyopo jijini Tanga.

"Tukio hili linaashiria kuanza rasmi kwa shughuli za mahakama kwenye mwaka husika na katika kuifanikisha tayari mahakama imeanza kuratibu utoaji wa elimu ya haki na sheria kwa umma ambapo mada mbalimbali huwasilishwa kupitia Radio na madawati maalum ya ushauri yaliyopo kwenye viwanja vya mahakama zote zilizopo kanda hii ili kuwapa fursa wananchi kushauriwa, kufahamishwa haki zao na kuelekezwa namna ya kuzidai kwa wakati ili kuharakisha maendeleo ,"alisema.

Aliongeza, "Mahakama baada ya kutekeleza maboresho katika utendaji wake wa kila siku hupokea mrejesho wa mara kwa mara kutoka kwa jamii na tumeona yapo mabadiliko makubwa katika miaka ya hivi karibuni ambapo wananchi wanaonesha mwamko wa kutafuta haki zao mahakamani tofauti na zamani, ".

Jiji Mfawidhi huyo alisema kuongezeka mahakamani kwa idadi ya kesi za jinai, mirathi na madai ni miongoni mwa viashiria vinavyothibitisha mafanikio hayo kutokana na mwendelezo wa mpango wa utoaji wa elimu ya haki na sheria kwa umma unaoratibiwa na Mahakama kwa kushirikiana na wadau wake kila mwaka.

"Jaji mfawidhi amesema Kesi nyingi hivi sasa hazichukui muda mrefu wa kusikilizwa kwasababu tumejiwekea lengo maalum kwamba ndani ya siku 90 uamuzi uwe umetolewa, kutokana na maboresho hayo imefikia wakati sasa baadhi ya mawakili wanalalamika kuhusu kasi hii tunayoenda nayo lakini hatuna namna ni lazima haki ipatikane kwa wakati ili kuwezesha ukuaji wa uchumi wa jamii na taifa kwa jumla, " alisema Jaji Aboud.

Aidha,  amesema mkuu wa mkoa wa Tanga, Martine Shigella anatarajiwa kutoa hotuba ya ufunguzi na hivyo kutoa wito kwa wakazi kujitokeza kwa wingi katika maadhimisho hayo.

Jumatano, 25 Januari 2017

TANROADS INABOMOA NYUMBA ZA BIASHARA 165,VIBANDA 84 MAILIMOJA KIBAHA PWANI.



WAKALA wa barabara (TANROADS)mkoani Pwani ,umeanza zoezi la bomoabomoa kuanzia eneo la Kiluvya Darajani hadi Mailmoja-Kibaha,ambapo limefanikiwa kwa asilimia zaidi ya 70 hadi sasa.

Zoezi hilo ni la siku tatu kuanzia Jan 23 hadi 25 lengo likiwa kupisha hifadhi ya barabara urefu wa mita 60.

Aidha bomoabomoa hiyo haitogusa eneo la soko la nafaka na baadhi ya mabucha ya nyama kutokana na soko jipya la nafaka kutokamilika hadi februari 15 hivyo kuendelea kusaidia wananchi kupata mahitaji yao muhimu.

Akizungumzia zoezi hilo linavyoendelea,meneja wa TANROADS Pwani,injinia Yudas Msangi,alisema wanalenga kubomoa nyumba za biashara 165,vibanda 84,nyumba za kuishi watu 10 na soko kuu la Mailmoja.

“Hadi kufikia leo mpango wetu unaenda vizuri sana ,tumeshafikia asilimia zaidi ya 70, na hii imetokana na kutokuwa na mtu wa kulalamika wala kuilaumu TANROADS”

“Tuliwapa taarifa mapema na wengi wametii kwa kuvunja wao wenyewe na kutoa vitu vyote vya thamani licha ya wachache ambao walishindwa kubomoa wao wenyewe,” alisema injinia Msangi.

Injinia Msangi,alieleza ,Maili Moja ndiyo imehitimisha zoezi la ubomoaji kwa watu waliojenga kwenye hifadhi ya barabara katika mkoa huo ambapo mwaka 2015 walibomoa maeneo mengine ya wilaya zote za mkoa.

Mkaguzi wa barabara, Injinia Livingstone Urio alisema huo ni mwendelezo wa usafishaji wa maeneo ya hifadhi ya barabara na kuweka usalama kwa wananchi kwani ni hatari kujenga ama kufanya biashara karibu na barabara.

Nae mkuu wa mkoa wa Pwani,mhandisi Evarist Ndikilo,alisema nia ya serikali sio kuona wananchi wanatangatanga bali ni kuwajengea mazingira na miundombinu bora ili waendeshe shughuli zao .

Alieleza kwamba ,hataki kuona mtu anajipenyeza kwenye maeneo ambayo tayari yamevunjwa.

Mhandisi Ndikilo alisema, Mji wa Kibaha umeshakua na kupanuka ukielekea kuwa manispaa hivyo hainabudi kufungua mianya ya kibiashara na njia kubwa za barabara ikiwemo Kisarawe na Bagamoyo  ili kuinua soko lake.

Diwani wa kata ya Mailmoja,Ramadhani Lutambi,alimpongeza mhandisi Ndikilo kwa kushirikiana na Tanroads kutoa elimu hivyo kuepusha malalamiko ambayo huwa yakijitokeza wakati wa bomoabomoa nchini.

Alisema haijawahi kutokea zoezi kama hilo likaenda kimya kimya na watu kuondoa vifaa vyao bila shuruti kama Mailmoja.

Hata hivyo,Lutambi alisema kuna changamoto imejitokeza kwa baadhi ya wafanyabiashara ambao wamekosa maeneo soko jipya la Mnarani,ambalo limetengwa na halmashauri.

Alibainisha kuwa soko jipya ni dogo, halitoshelezi mahitaji,frem za biashara zilizobomolewa ni 165,zilizopo 110 sokoni hapo huku wajasiriamali wakiwa ni 400 na soko hilo likiwa na nafasi aya watu 200.

Lutambi alisema, lazima wengine watakosa nafasi na ndio maana malalamiko ni makubwa hivyo anawasiliana na halmashauri,wilaya na mkoa ili kuona namna ya kusaidia watakaokosa na kutenda haki bila upendeleo.

Jumanne, 24 Januari 2017

MKUU WA WILAYA YA LUSHOTO AGIZA WAKAMATWE WAZAZI AMBAO WAMEWAZUIA WATOTO WAO KWENDA SHULE.



MKUU wa wilaya ya Lushoto January Lugangika ametoa siku 14 kwa wanafunzi waliotakiwa kuripoti shule kwa ajili ya kuanza masomo ya kidato cha kwanza wawe wamefanya hivyo kabla ya hatua za kisheria dhidi yao hazijachukuliwa.

Agizo hilo alitoa Mara baada ya kufanya ziara ya ukaguzi wa miundombinu ya ujenzi wa maabara katika shule ya sekondari ya Bernard Membe iliyopo katika kata ya Kwakanga wilayani humo.

Alisema kuwa shule hiyo ilipangiwa wanafunzi 90 lakini toka shule zilipofunguliwa mpaka sasa  ni wanafunzi Tisa pekee ndio waliweza kuripotia kwa ajili ya kuanza masomo shuleni hapo huku 81 wakiwa hawajaripoti.

" Lugangika amemwagiza mwenyekiti wa kijiji kwa kushirikiana na mgambo wawakamateni wazazi ambao watoto wao hajaripoti shule wahojini na wakishindwa kuripoti shule basi nileteeni taarifa tuwapeleka mahakamani wazazi wote ambao watoto wao wamefaulu na wameshindwa kiwapeleka shule".

Aidha katika hatua nyingine aliagiza baada ya wiki mbili kupita wazazi wote ambao watashindwa kutoa ushirikiano ikiwemo kupeleka watoto wao shule basi wapelekwe mahabusi.

Hata hivyo Mkuu wa shule hiyo ya Sekondari Boniface Winifred's wakati akitoa taarifa ya maendeleo ya shule hiyo alisema kuwa shule hiyo inakabiliwa na uhaba mkubwa wa walimu hususani wa masomo ya sayansi.

Alisema kuwa hali hiyo inachangia kwa kiasi kubwa uwepo wa utoro kwa wanafunzi na wale wapya kuvunjika moyo wa kuja kupata elimu katika shule hiyo.

"Changamoto nyingine muindombinu iliyopo sio rafiki kwa mwanafunzi wala walimu kuweza kufanikisha lengo la utoaji wa elimu kwani kuna mpaka uhaba wa madarasa pamoja na vitabu vya kiada " alisema Mwalimu hiyo.


Alhamisi, 19 Januari 2017

WAZIRI MKUU KASSIMU MAJALIWA AMALIZA MGOGORO WA MPAKA KATI YA KILINDI NA KITETO NA KUWATAKA VIONGOZI WA SIASA WAACHE KUWAVURUGE WANANCHI





Waziri Mkuu akiwa kwenye ziara ya kutembelea mpaka wa Tanga na Manyara na akizungumza na viongozi kiwepo mkuu wa Mkoa wa Manyara mkuu wa mkoa wa Tanga waziri wa ardhi pamoja na wananchi. 
 

 
HABARI.
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameumaliza mgogoro wa mpaka wa ardhi baina ya vijiji vya wilaya za Kiteto na Kilindi uliodumu kwa muda mrefu.

Mgogoro huo ambao ulianza kusuluhishwa tangu mwaka 1997, umepata suluhu kwenye mkutano wa hadhara uliohutubiwa na Waziri Mkuu na kuwajumuisha Wakuu wa Mikoa hiyo miwili, Wabunge wa Kiteto na Kilindi, wenyeviti wa Halmashauri na madiwani wa kata mbili za mpakani pamoja na wananchi wa kata hizo.

Waziri Mkuu pia amewataka wanasiasa na viongozi wengine kutowavuruga wananchi na badala yake wawaongoze vizuri na kutoa maelekezo kwa mujibu wa sheria za nchi.

Ametoa agizo hilo jana (Jumatano, Januari 18, 2017)  wakati akizungumza na wananchi wa wilaya za Kiteto na Kilindi katika kijiji cha Lembapili wilayani Kiteto, mkoani Manyara ambako ni kuna mpaka wa  wilaya hizo mbili alipokwenda kutatua mgogoro huo.

Alisema viongozi wa wilaya hizo lazima wafuate sheria na wawaelekeze wananchi umuhimu wa kuzingatia sheria za nchi ikiwa ni pamoja na kuheshimu mipaka iliyowekwa kwa mujibu wa sheria ili kuepusha migogoro.

Akizungumzia kuhusu mgogoro huo wa mpaka, Waziri Mkuu alisema nchi ilishaweka mipaka ya mikoa na wilaya zake yote tangu zamani na kumbukumbu zipo zikiwemo za mpaka wa  wilaya hizo tangu mwaka 1961 kwa  tangazo la Serikali namba 65 na hakuna mabadiliko. Hivyo, aliwasisitiza wauheshimu na kuufuata.

Alisema Serikali kupitia Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi itakwenda kuweka alama vizuri na viongozi wa wilaya hizo watashirikishwa. Alama hizo zitawekwa na kifaa maalumu, hivyo amewataka wahusika watoe ushirikiano.

Waziri Mkuu alisema katika kipindi ambacho Serikali itakuwa ikiweka alama hizo, wananchi waendelee na shughuli zao hadi hapo zoezi litakapokamilika na wala wasibughudhiwe.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ametoa siku nane kwa watu wote wanaomiliki silaha katika wilaya za Kilindi na Kiteto wazipeleke kwenye vituo vya Polisi ili zisajiliwe upya na kisha Wakuu wa Mikoa wafanye operesheni maalum na atakayekutwa anamiliki silaha kinyume cha sheria achukuliwe hatua.

“Wakuu wa Mikoa fanyeni ukaguzi maalum na atakayekutwa anamiliki silaha kinyume na utaratibu achukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria. Pia kuna watu wana mitambo ya kutengenezea bunduki hapa, nao pia waisalimishe haraka,” alisisitiza.

Kwa upande wake, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Bw. William Lukuvi alisema mwanzoni mwa Februari wataalamu wake watakwenda katika mpaka huo ili kuanza kuweka alama vizuri.

Alisema baadhi ya viongozi huwa wana tabia ya kuzuia watendaji kutekeleza majukumu yao, hivyo ametumia gursa hiyo kuwaomba viongozi wa wilaya hizo watoe ushirikiano.

Alisema moja ya majukumu aliyopewa na Mheshimiwa Rais, Dk. John Pombe Magufuli ni kuhakikisha ndani ya miaka hii mitano anamaliza migogoro ya ardhi nchini ukiwemo huo wa Kilindi na Kiteto.

Jumatano, 18 Januari 2017

KAIMU KATIBU MTENDAJI WA TUME YA MIPANGO, FLORENCE MWANRI AFANYA ZIARA KUANGALIA SHUGHULI ZA UZALISHAJI WA SARUJI KATIKA KIWANDA CHA TANGA CEMENT.





Meneja wa Kiwanda cha Tanga Cement, Mhandisi Ben Lema mwenye Miwani, akimwonesha Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango, Bibi Florence Mwanri  Wengine ni Maofisa wa Ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo walioambatana na Kaimu Katibu Mtendaji katika ziara hiyo.

Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango, Bibi Florence Mwanri akikagua mifumo ya kisasa inayotumika kuendesha shughuli mbalimbali katika kiwanda cha Tanga Cement.
 Baadhi ya mitambo inayoendelea kufanya kazi katika kiwanda cha Tanga Cement.

 
 
TANGA

Timu ya ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo kutoka Tume  ya Mipango ikiongozwa na Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume hiyo, Bibi Florence Mwanri imefanya ziara katika Kiwanda cha Tanga Cement kilichopo Mkoani hapa kwa lengo la kukagua shughuli mbalimbali zinazofanywa na kiwanda hicho.

Katika ziara hiyo, Bibi Mwanri amepata fursa ya kukagua maeneo mbalimbali ya kiwanda hicho ikiwa ni pamoja na eneo linalotumika kuchimba malighafi za kutengenezea saruji, teknolojia ya kisasa inayotumika kuendesha mashine kiwandani hapo pamoja na kuangalia hatua mbalimbali zinazotumika katika uzalishaji wa saruji.

Akiwa katika eneo linalochimbwa mawe ya kutengenezea saruji, Mwanri ameeleza kuwa kiwanda hicho kina wajibu wa kuhakikisha sheria  na taratibu za utunzaji wa mazingira zinazingatiwa muda wote ili kuhakikisha mazingira yanabaki salama licha ya shughuli za uchimbaji kuendelea kufanyika.

Mwanri amepongeza uongozi wa kiwanda hicho kwa kuendelea kutekeleza majukumu yake katika kuunga mkono dhamira ya Serikali ya kuwa nchi ya Viwanda na kuharakisha malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo inayosisitiza kufikia uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.

Naye Meneja wa Kiwanda hicho, Mhandisi Ben Lema amesema kiwanda hicho kimeendelea  kutoa ajira kwa watanzania katika kada mbalimbali ambapo kwa sasa kua ajira zaidi ya 600 ambapo ajira 300 ni za moja kwa moja huku ajira 300 zingine ambazo sio za moja kwa moja zinajumuisha wauzaji, wasambazaji, wasafirishaji na wengine walioko katika mnyororo huo.

Ameongeza kuwa bidhaa za kiwanda hicho bado zinafanya vizuri sokoni licha ya ushindani uliopo kufuatia kuanzishwa kwa viwanda vingi vinavyozalisha saruji kwa kuwa mahitaji ya saruji bado ni mwakubwa sokoni.



Lema amesema viwanda vya saruji vinapata faraja kubwa kwa kuwa miradi mbalimbali ya ujenzi inayotekelezwa na Serikali na hata inayotekelezwa na sekta binafsi inatumia saruji inayotengenezwa na viwanda vya ndani ya nchi.