Askari
na Maafisa wa jeshi la Polisi nchini wameaswa kutotumia madaraka yao
vibaya kwa kuwabambikizia wananchi kesi kwani kufanya hivyo ni kushindwa
kusimamia dhamira njema ya Mhe Rais ya kuwapatia wananchi wanyonge haki
zao stahiki.
Hayo
yamesemwa na Waziri wa Mambo ya ndani ya nchi Mhe Mwigulu Nchemba
wakati akifungua kikao cha kazi cha Siku tatu cha mwaka 2017 kwa maafisa
waandamizi wa Polisi na Makamanda wa Mikoa/Vikosi kilichofanyika katika
ukumbi wa Mikutano wa LAPF Mjini Dodoma.
Mhe
Mwigulu amesema kuwa kumekuwa na malalamiko kutoka kwa wananchi juu ya
kuwabambikizia kesi, Kuwabadilishia watu kesi zao za msingi kwa sababu
ya kushindwa kutoa rushwa hivyo kikao hicho kinapaswa kuwa na maamuzi na
maadhimio yenye dira na taswira njema kwa jamii na Taifa kwa ujumla.
Amesisitiza
pia Askari na Maafisa wa Polisi kutotumia taarifa za watu wanaohasiana
kuwa ndio chanzo pekee cha msingi wa shtaka badala yake kufanya
uchunguzi kwa kina na kujiridhisha vyema ili kufikia hukumu yenye tija
Na haki kwa mtuhumiwa kwani kufanya hivyo kutaimarisha amani na jeshi la
Polisi kupata taarifa nyingi za uhalifu kutoka kwa wananchi endapo
watajikita katika haki.
Akizungumzia
Vita dhidi ya Dawa za Kulevya Mhe Nchemba alisema kuwa serikali
imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kukamata na kuziteketeza Dawa za kulevya
zilizopo mashambani ambapo ametilia msisitizo zaidi kwa Askari na
Maafisa wa Jeshi la Polisi kuendelea kupambana ili kuzikamata Dawa za
kulevya zilizopo katika viwanda.
Amesisitiza
pia Jeshi la Polisi kuendelea kupambana na kubaini uhalifu sambamba na
kushirikiana na vyombo vingine ili kuhakikisha lengo mahususi la
serikali ambalo ni kuzuia uhalifu linafanikiwa kwa kiasi kikubwa.
Mhe
Mwigulu amesema kuwa kauli mbiu ya Mwaka 2017 inayosema “ZINGATIA
MAADILI TUNAPOPAMBANA NA UADILIFU ILI KUIMARISHA USALAMA KWA MAENDELEO
YA TAIFA” endapo kama itatekelezwa kwa vitendo itaijenga nchi na kuzidi
kudumisha zaidi amani iliyopo kwa wananchi.
Naye
Kamanda wa Jeshi la Polisi nchini Ernest Mangu alisema kuwa kikao hicho
cha kazi kwa Maafisa wa Jeshi la Polisi kina dhamira kubwa ya kufanya
Tathmini ya utendaji wa mwaka 2016 na kuandaa mikakati mizuri ya mwaka
2017 na kupata fursa ya kubadilika kiutendaji kwa kuzingatia dhamira ya
serikali ya awamu ya Tano inayoongozwa na Mhe Rais Dkt John Pombe
Magufuli.
Hata
hivyo amesisitiza zaidi askari wote nchini kutofanya kazi kwa mazoea,
Kuacha Urasimu na kujenga uaminifu na weledi katika kazi.
Mangu
amesema matendo ya Askari Polisi nchini yanapaswa kuwa mfano bora wa
kuigwa katika jamii hivyo askari Polisi hapaswi kuwa chanzo cha vurugu
au kujihusisha na matendo ovu yasiyostahili katika jamii.
Ameongeza
kuwa miongoni mwa mambo yatakayopewa kipaombele kwa kujadiliwa katika
Kikao hicho itakuwa ni pamoja na Vita dhidi ya Dawa za Kulevya, Vita
dhidi ya Magendo, Vita dhidi ya ujangili na Uvuvi sambamba na Vita dhidi
ya Ubambikizaji wa kesi kwa wananchi.
Kwa
upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe Jordan Lugimbana akitoa salamu
za Mkoa wa Dodoma kabla ya kumkaribisha Waziri Mwigulu Nchemba
kuzungumza na askari hao amelipongeza jeshi la Polisi kwa kazi kubwa
linayofanya ambapo pia ameeleza mpango wa Mkoa katika kupambana na
migogoro ya ardhi kwa kuanzisha kamati maalumu ya wataalamu wa sheria
kutoka chuo kikuu cha Dodoma (UDOM) Kupitia na kushauri ili kuweza
kumaliza haraka migogoro hiyo.
Naye
Makamu wa kwanza wa Rais na Waziri Mkuu Mstaafu Mzee John Samwel
Malecela alisema kuwa jambo la msingi ambalo askari Polisi wanapaswa
kulifanya ni pamoja na kuhakikisha kila mwananchi anapata Uhuru wake na
kama jambo hilo likitekelezwa ipasavyo Fikra za Hayati Mwalimu J.K
Nyerere zitakuwa zimeenziwa kwa weledi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni