WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame
Mbarawa, amezitaka Kampuni za Mawasiliano kukamilisha taratibu za usajili
katika Soko la Hisa la Dar es Salaam kwa kuuza asilimia 25 ya hisa zote kadri
ya Sheria ya Masoko ya Mitaji na Dhamana inavyoelekeza mwishoni mwa mwaka huu.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Prof. Mbarawa
ametaja kampuni hizo kuwa ni zile zenye leseni za mawasiliano zilizotolewa
kabla ya tarehe 1 Julai 2016 kwa ajili ya Miundombinu ya Mawasiliano, Huduma za
Mawasiliano, na Huduma za Matumizi.
“Watoa huduma wote wa Mawasiliano wajisajili na
kuuza hisa zao kwa wananchi ndani ya mwezi wa Disemba”, amesema Waziri Prof.
Mbarawa.
Ameongeza kuwa kwa Kampuni zilizopata leseni baada
ya tarehe mosi Julai, 2016 watatakiwa kutimiza sharti hilo la kisheria kwa
kipindi kisichozidi miaka miwili tangu kusajiliwa.
Waziri Prof. Mbarawa amesisitiza kuwa Kampuni
zitakazokiuka Sheria hiyo zitachukuliwa hatua za kisheria kupitia kifungu cha
21 (C) cha EPOCA, 2010.
Aidha, amewataka wananchi kutumia fursa hiyo kununua
hisa hizo na kuwa sehemu ya wamiliki wa makampuni ya Mawasiliano ili kuongeza
kipato na kushiriki katika maamuzi ya kampuni hizo.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni