Jumanne, 6 Desemba 2016

JESHI LA POLISI MKOA WA TANGA LAFANIKIWA KUMKAMATA ASKARI ANAYETUHUMIWA KUMUUWA ASKARI MWEZIE.



POLISI mkoani Tanga imefanikiwa kumkamata na kumfukuza kazi askari wake, Konstebo Maiko Komba aliyekuwa ametoroka kituo cha kazi kwa siku takriban 20, baada ya kuhusishwa na mauaji ya mpenzi wake ambaye naye alikuwa askari mkoani humo.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, David Mnyambuga amebainisha hayo wakati akitoa taarifa kwa vyombo vya habari ofisini kwake jana.

Mnyambugha alisema Komba alitoroka kazini Novemba 13, mwaka huu baada ya kudaiwa kumpiga hadi kumsababishia kifo mzazi mwenzake ambaye pia ni askari aliyekuwa na namba WP 9504, Elizabeth Nnko  katika tukio lililofanyika jijini Tanga.

“Baada ya Polisi Tanga kupata taarifa za chanzo cha tukio la kifo cha WP 9504 Elizabeth Nnko kwamba ni ugomvi wa kimapenzi uliokuwa ukiendelea kati yake na mzazi mwenzie Konstebo Maiko Komba tayari alikuwa amekimbilia kusikojulikana hivyo hatukufanikiwa kumpata,” alieleza Kaimu Kamanda.

Kaimu Kamanda Mnyambuga alisema baadaye Jeshi la Polisi Tanga liliendelea kufanya uchunguzi ili kufuatilia askari huyo na hatimaye kupitia taarifa za wasamaria wema ilibainika kwamba Komba alikuwa amejificha jijini Dar es Salaam.

“Juzi Desemba 3, mwaka huu saa sita mchana huko Kiwalani Minazi Mirefu jijini Dar es Salaam askari wetu wa upelelezi wa hapa Tanga kwa kushirikiana na waliopo huko walifanikiwa kumkamata Komba na kumrejesha jijiji hapa akiwa chini ya ulinzi na mpaka sasa bado tunaendelea kumhoji,” alisema Kamanda Mnyambuga.

“Kwa sasa Jeshi la Polisi Tanga limemfukuza kazi kutokana na kosa la utoro kazini na kuhusu tuhuma za kosa la mauaji bado upelelezi dhidi yake unaendelezwa na huenda atafikishwa mahakamani mara baada ya uchunguzi kukamilika.”


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni